Waziri wa Afya , Ustawi wajamii ,Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui akizungumza na uongozi kutoka Hospitali ya PUSHPAWATI iliopo Nchini India mara walipofika ofisini kwake kujitambulisha.
Waziri wa Afya , Ustawi wajamii ,Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui (kushoto) akimkabidhi Meneja wa masoko ya Kimataifa hospital ya PUSHPAWATI iliopo Nchini India Sanoj Kumar (katikati) kitabu cha kumbukumbu ya Zanzibar mara walipofika ofisini kwake kujitambulisha, wamwanzo kulia ni Mjumbe kutoka Hospitali hiyo Ratnesh Sinha.
Na Issa Mzee – Maelezo
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui amesema wizara yake inatarajia kushirikiana na Hospitali ya Pushpawati singhania ilioko Delhi nchini india katika kuwapatia matibabu bora wananchi wa Zanzibar.
Alisema hayo ofisini kwake Mnazi Mmoja Mjini Unguja, wakati alipokutana na uongozi wa Hospitali hiyo uliofika wizarani hapo kwa ajili ya kujitambulisha.
Alisema hospitali hiyo itasaidia katika kuwapatia wananchi huduma mbalimbali za matibabu ikiwemo moyo, matatizo ya haja ndogo pamoja na upandikizaji wa figo.
Alieleza kuwa, hospitali hiyo imeamuwa kwa makusudi kushirikiana na Zanzibar katika huduma za afya ili kuwasaidia madaktari wa Zanzibar waweze kupata ujuzi na uzoefu wa kutumia mashine za kisasa na kufanya uchunguzi wa maradhi mbalimbali ya binadamu.
Aidha alisema, hatua inayofuata ni kuandaa taratibu za kusaini hati ya makubaliano baina ya Wizara hiyo na Hospitali ya Pushpawati kwa lengo la kuanza kusaidia huduma za matibabu nchini.
Nae Meneja wa Masoko ya Kimataifa wa Hospitali hiyo, Sanoj Kumar amesema ipo haja ya kuwaleta wataalamu wao Zanzibar ili kusaidia utoaji wa huduma za matibabu kwa wananchi.
Alisema ushirikiano huo pia utasaidia katika kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa wanaokwenda nchini india kwa ajili ya matibabau.
Aidha alisema Hospitali ya Pushpawati singhania, itaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali ili kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana Zanzibar.