Sunday, November 24

Changamoto iliyojitokeza kukosekana kwa maji ipatiwe ufumbuzi haraka – Dk Hussein Mwinyi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameigiza Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha changamoto iliyojitokeza ya ukosefu wa maji kwa baadhi ya maeneo ya Mji wa Zanzibar inapatiwa ufumbuzi wa haraka ili wananchi waendelee kupata huduma hiyo ipasavyo.

Dk. Mwinyi ametoa agizo hilo leo wakati alipotembelea na kukagua vyanzo vya Mradi wa Maji unaopeleka huduma hiyo Mjini Zanzibar ambapo miundombinu yake imeharibika na kusababisha kukosekana kwa huduma hiyo katika maeneo mbali mbali ya Mji wa Zanzibar kwa takriban siku nne sasa.

Rais Dk. Mwinyi aliwataka watendaji wa (ZAWA) kuongeza kasi katika utatuzi wa changamoto za maji zinazoukabili mji, akibainisha matumaini yake baada ya baadhi ya vifaa, ikiwemo mabomba kuwasili.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameitaka Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kutengeneza mfumo utakaowawezesha wananchi wa maeneo ya Miwani, Kizimbani na Bumbwisudi kupata huduma za maji kupitia  Mradi wa Maji safi na salama unaopeleka huduma hiyo Mjini Zanzibar.

Alisema kuna umuhimu wa (ZAWA) kuaandaa mfumo maalum kutoka kisima kimoja miongoni mwa Visima saba vilivyopo, ili wananchi wa maeneo hayo  waweze kupata huduma hiyo ya maji.

Alisema mradi huo wakati unaanzishwa haukuzingatia mahitaji ya wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka vyanzo hivyo, na hivyo kuwafanya  kukosa kabisa huduma hiyo.

Aidha, alisema Serikali hivi sasa ina mpango wa utekelezaji wa miradi mbali mbali ya barabara na umeme, hivyo akawahakikishia wananchi wa maeneo hayo kuwa Serikali  itashughulikia changamoto zinazowakabili.

Dk. Mwinyi aliwataka wananchi hao kuwa wastahamilivu katika kipindi hiki cha kiangazi, sambamba na kuwataka kumuomba Mwenyezi Mungu ili awaletee neema ya mvua na kuendeleza kilimo mashambani.

Vile vile, aliwashukuru Mafundi wa (ZAWA) kwa kufanikiwa kurejesha mfumo uliosababisha kuunguka kwa mabomba na kusababisha ukosefu huo wa maji.

Mapema, Mkurugenzi wa (ZAWA) Dk. Salha Mohamed Kassim alisema kazi kubwa zinazofanywa na Mamlaka hiyo  zinahitaji gharama kubwa na kubainisha mpango maalum ulioandaliwa wa kulipa madeni, ikiwemo ya walinzi wa kiraia kwenye visima vya maji.

Aliwahakikishia wananchi hao kuwa wale wote wanaoidai Mamlaka hiyo watapatiwa haki zao hivi karibuni.

Nao, baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na vyanzo hivyo, walionyesha masikitiko yao kwa kukosa huduma za maji safi na salama kwa kipindi chote tangu mradi huo unaopeleka maji Mjini kuanzishwa, ingawa vyanzo vya huduma hiyo inapatikana katika maeneo yao.

Aidha, walilamika kuwepo kwa barabara mbovu kuelekea katika Shehiya zao pamoja na ukosefu wa huduma za umeme changamoto ambazo Rais Dk. Mwinyi aliwahakikishia kwamba zitapatiwa ufumbuzi.

Imetayarishwa na

Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar