NA ABDI SULEIMAN.
CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), kimewataka waandishi wa habari za uhifadhi, uwindaji haramu na usafirishaji wa wanyamapori Tanzania, kuhakikisha wanayashirikisha makundi yote wakati wa kuandika habari hizo.
JET imesema wakati umefika katika kuandika habari hizo kuyashirikisha makundi yote yanayohusika ikiwemo wanawake, watoto, wazee na Vijana.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET) John Chikomo, wakati akifungua mafunzo juu ya kuongeza uwelewa wa waandishi wa habari, juu ya biashara ya wanyamapori kubadilisha tabia ya jamii kuelekea utumiaji wa wanyamapori haramu, kupitia taasisi ya TRAFFIC ya Afrika Mashariki.
Alisema waandishi wananafasi kuwa kuyatumia makundi hayo katika habari zao, ili kuona yanapata nafasi kubwa kwani wamekuwa ndio wahanga pale yanapotokea matukio ya uwindaji haramu ya wanyamapori.
Naye Mwenyekiti wa JET Dr.Ellen Otaru, alisema kazi kubwa iliyopo ni kutoa elimu na ushirikishwaji wa vijana na wanawake, katika ulinzi na uhifadhi wa mazingira na maliasili kwa maendeleo endelevu, kwani vijana ndio tegemeo la taifa na wanaongezeka.
“Watanzania wanafikia Milioni 60 wakiwemo wanawake na Vijana, vijana wao wanafikia 40% ya watu ndio walengwa wa taifa, ardhi ipo pale pale haiongezeki, ujenzi unaendelea, barabara zinajengwa na miji inakuwa, hali inayopelekea kugusa maeneo ya uhifadhi maliasili, ifike wakati tuwe na maeneo maalumu kwa ajili ya uhifadhi”alisema.
Alisema matumizi mabaya ya mazingira hupelekea wanyama na viumbe mbali mbali kupotea na baadhi yao kufariki, hayo yanatokana na matumizi mabaya ya mazingira yanayofanywa na binaadamu.
Akiwasilisha mada kuhusu Mtandao wa ufuatiliaji wa biashara ya wanyamapori na muhtasari wa Biashara haramu ya wanyamapori duniani kote, Afirika Mashariki na Tanzania, afisa Ufuatiliaji wa biashara hiyo Allen Mgaza, alisema lengo ni kuongeza uelewa wa habari juu ya biashara haramu ya wanyamapori kwa kubadilisha tabia ya jamii kuelewa utumiaji wa wanamapori na haramu.
Alisema katika ufuatiliaji uharibifu wa mazingira na maliasili, wamebaini kundi kubwa la wanawake na vijana halina uelewa mpana wa elimu ya uhifadhi wa mazingira na maliasili na kubaki, kupoteza hamasa ya kuisaidia jamii na mamlaka katika uendelezaji wa tunu hiyo ya taifa.
“Juhudi na sheria mbali mbali za udhibiti wa uhifadhi wa mazingira na maliasili, bado elimu inapaswa kutolewa tokea ngazi za skuli, ili kuona wanawake na vijana wanapata uelewa wa kutosha juu ya ulinzi wa rasilimali hizo”alisema.
Nae Meneja wa mabadiliko ya Tabia kutoka taasisi ya Traffic Afrika ya Mashariki Jane Shuma, akiwasilisha mada juu ya mipango ya mabadiliko ya Tabia kuelekea ulaji wa wanyamapori, alisema biashara ya wanyamapori isipofuata sheria ni biashara haramu hiyo, hivyo walaji wa wanyapori wanapaswa kuwa makini katika ulaji wa wanyama hao.
Nao waandishi wa habari hizo, wamesema wakati umefika kwa mashirika na taasisi za serikali kuelekeza nguvu zaidi katika kutokomesha biashara haramu ya wanyamapori nchini.
MWISHO