NA ABDI SULEIMAN.
BALOZI wa CANADA nchini Tanzania Pamela O’Donnell, amesema hakuna maendeleo yenye maana, yawe ya kibiashara, kijamii au kidiplomasia yanayowezekana bila ushiriki kamili na usawa wa wanawake nchini.
Hivyo alisema ni jukumu la kila mmoja kuhamasisha uwezeshaji wa wanawake, pia wananafasi sawa ya kufanikiwa na wanaweza kuwa makada wazuri wa mabadiliko, huku utafiti ukionyesha kwamba wanawake wanapofanya kazi uchumi unakuwa.
“Uwezeshaji wa wanawake kiuchumi unakuza uzalishaji, unaongeza mtawanyiko wa uchumi na usawa wa kipato zaidi, hali inayowafanya wanawake kuonekana kuwa watu wa kukuza uchumi”alisema.
Alifahamisha kuwa Canada ni mdhamini wa muda mrefu wa harakati za wanawake na wanaendelea kushika kasi duniani, ili kuona usawa wa kijinsia uwezeshaji wa wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu na kufikia haki za binaadamu.
Balozi Pamela alisema uwezeshaji wa wanawake kijinsia na wasichana, kunachangia sana katika kuongeza kasi ya kupunguza umasikini na kuongeza maendeleo endelevu, kwani uzinduzi wa mradi huo uweze kuvunja vizingiti vinavyowakabili wanawake, wasichana na wenye ulemavu kutokuwacha nyuma katika jitihada za kuleta maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, alisema serkkali inadelea na juhudi a kuhakikisha za kuwafikia makundi yote, kubadilisha maisha ya watu lakini juhudi hizo zinahitaji kuungwa mkono na wadau wa maendeleo.
Alisema uzinduzi wa mradi huo wakuwasaidia akinamama katika masuala ya kiuchumi, hivyo asasi za kiraia zina mchango mkubwa wakusaidia juhudi za serikali.
“Serikali ina malengo ya kuleta maisha na kwa wanachi, hivyo serikali inahitaji ushirikiano wa mataifa mengine, ili kuweza kuifikia azma yake hiyo”alisema.
Mkurugenzi wa Vijana Hai Foundation Erick Godfrey Ramsey, alisema mradi unakusudia kutoa mafunzo kwa wanawake 60 juu stadi za maisha, ujuzi wa kifedha, ujasriamali, masuala ya mawasiliano, ili kuona wanawake wanafikia malengo yao yaliokusudiwa.
Alisema lengo ni kuwahamasisha wanawake vijana, wajane na watu wenye ulemavu ili kuweze kujitengemea kimaisha na kuachana na utegemezi.
Kwa upande wake Mrajis wa NGOs Zanzibar Ahmed Khalid Abdullah, alisema mradi huo umelenga kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuwakwamua na umaskini.
MWISHO