Wednesday, October 30

Ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu kwenye mambo mbali mbali ndio njia pekee yakuleta usawa katika jamii.

Na, Hassan Msellem, Pemba.

Mwenyekiti wa Baraza la watu wenye ulemavu Zanzibar, Salma Hajji amesema watu wenye ulemavu wanapaswa kushirikishwa kwenye mipango yote ikiwemo ya kisera hasa kwa masuala yanayohusu kundi hilo.

Akitoa taarifa ya kuelekea maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Disemba 3 ya kilamwaka, amesema si jambo busara iwapo Jamii itawatenga na
kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu kwa kutowashirikisha katika masuala mbalimbali ikiwemo hata yale yanayowahusu.

Ameongeza kuwa ili kuhakikisha watu wenye ulemavu
wanapata maendeleo ni lazima wajumuishwe katika Nyanja zote
zikiwemo za kisiasa, Kijamii na kiuchumi.

Aidha amewasihi wanahabari kuwa mabalozi wazuri na kuifanyia kazi kwa vitendo kaulimbiu ya mwaka huu ambayo ni “uongozi na
Ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu, kuelekea ujumuishwaji na ufikiwaji endelevu baada ya Uviko-19 Duniani.”

Amesema hatua hiyo itasaidia kufikia sera ya Serikali ya awamu ya nane ya uchumi wa buluu wenye neema na mafanikio kwa
watu wenye ulemavu na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wa Zanzibar maadhimisho ya watu wenye ulemavu kwa mwaka huu yatafanyika Disemba 4 kwenye kiwanja cha
Hamburu huko Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.