Wednesday, October 30

WALIOKUFA KWA KULA KASA WAONGEZEKA SASA WAFIKIA WATU 7

 

NA MWANDISHI WETU.

Jumla ya watu Saba (7) wakaazi wa Msuka Wilaya ya Micheweni Pemba wametariki Dunia kwa muda siku mbili tafauti baada ya kuaminika wamekula samaki aina ya kasa anaesadikiwa kuwa na Sumu.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib amewataka wananchi kila anaejuwa amekula samaki huyo kukimbilia Hospital kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Aliyaeleza hayo huko katika maeneo ya waathirika hao baada ya kwenda kuwafariji na kuangalia Hali za wagonjwa walioko hospital ya Micheweni.

Alisema kuwa Serikali haina nia ya kuwaadhibu wananchi ambao wamekula  samaki huyo Bali inania ya kuokowa maisha yao kwa vile Kuna wenzao wameshapoteza maisha.

“Sisi kama Serikali hatuna nia ya kuwaadhibu wananchi ambao wamekula samaki huyo  waondowe hofu hiyo ispokuwa tunataka kuokowa maisha yao”, alisema.

Kwa upande wake Ofisa mdhamini Wizara ya Afya ,Ustawi wa jamii,jinsia wanawake na watoto Pemba Yakoub Moh’d Shoka aliwataka waathirika kutowa ushirikiano na Wizara ya Afya kwa kujitokeza kwenda Hospital kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu ili kuondowa sumu iliyo mwilini kwa kula Samaki huyo.

Alisema tayari Wizara yake imeshachuwa vipimo vya damu  za baadhi ya waathirika hao kwa ajili ya kunifanyia uchunguzi wa kitaalamu kwenye maabara ya mkemia Kisiwani Pemba.

“Tunawaomba wananchi ambao wamekula samaki huyo kukimbilia Hospital kwa ajili ya kutupa ushirikiano kwa kuwapatia matibabu na vipimo ili kujuwa tatizo lililo wadhuru”, alieleza.

Nae daktari dhamana wa Hospital ya Micheweni Pemba Zubeir Omar Zubeir akitowa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alisema jumla ya wagonjwa 63 walishapokelewa hospitalini hapo tokea kutokea kwa mkasa huo.

Alieleza kati ya hao wagonjwa 29 walipatiwa matibabu na kuruhusiwa  kurejea majumbani kwa siku ya jumaamosi wagonjwa 34 walilazwa.

“Kati ya wagonjwa tuliowapokea watatu (3) walifariki Dunia siku ya jumaamosi na leo jumaapili asubuhi wengine wawili kati ya hao tuliowalaza wamekufa pia,” alieleza.

Hata hivyo wanawaomba wananchi kila anaehisi ni muathirika kukimbilia Hospital kwani wengine wametariki majumbani kwao kwa kukosa matibabu.