NA ABDI SULEIMAN.
MASHEHA wa Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, wamelitaka shirika la umeme Zanzibar ZECO Tawi la Pemba, kuacha kuwafumbia macho wanaoharibu miundombinu ya umeme na kupelekea kulitia hasara shirika na serikali kwa ujumla.
Walisema kumekuwa na wananchi huharibu miundombinu ya umeme kwa makusidi, pamoja na wanaiba umeme kwa kujiungia kinyume na sheria jambo ambalo limekua likiendelea kutokea mara kwa mara.
Masheha hao waliyaeleza hayo wakati wa kikao maalumu cha kuorodhesha vijiji ambavyo havijafikiwa na huduma ya umeme, ili waweze kupatiwa huduma hiyo kama vilivyo vijiji vynengine.
Mrisho Juma Mtwana sheha wa shehia ya Mtemani, alisema shirika la umeme ZECO linapaswa kuwachukulia hatua wale weote wanaoharibu miundombinu ya umeme katika laini kubwa, sambamba na wanaojiungia huduma hizo bila ya kufuata taratibu.
Alisema katika shehia yake hakuna kijiji hata kimoja, ambacho hakijafikiwa na huduma ya umeme tatizo ni wizi wa umeme unaofanywa na baadhi ya wananchi kinyume na sheria.
Ali Khatib Chwaya sheha wa shehia ya selemu, alilitaka shirika la umeme ZECO kujipanga kikamilifu katika suala la kukatika umeme mara kwa mara, kwani tayari wawekezaji wameshaanza kujitokeza na umeme ndio tegemeo lao kubwa.
Naye sheha wa shehia ya Kiungoni sheha wa shehia ya Kiungoni, aliwataka ZECO kuhakikisha wanafika vijijini kutoa elimu kwa jamii juu ya suala zima la matumizi ya umeme.
Afisa uhusiano wa shirika hilo tawi la Pemba Amour Salum Massoud, alisema hali ya upatikanaji wa huduma ya umeme katika wilaya ya Wete iko vizuri, huku juhudi za ziada zikiendelea kuchukuliwa ili huduma hiyo iendelea kuwa bora.
Alisema changamoto kubwa ni hujuma za miundombinu ya huduma ya umeme, wananchi kuharibu kwa kuchimba mchanga, kukata miti karibu na nyaya za umeme, kuchoma moto pamoja na ungaji wa umeme kinyume na taratibu.
Kwa upande wake afisa Mipango na utafiti ZECO Pemba Ali Faki Ali, alisema wilaya ya Wete jumla ya Vijiji 106 sawa na 95.5% vimeshapatiwa umeme, huku vijiji vitano ndio bado havijapatiwa huduma hiyo.
Alisema mikakati yao ni kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa na huduma hiyo na hakuna kijiji ambacho kitakua hakina hudma ya umeme.
MWISHO