NA ZUHURA JUMA, PEMBA.
WATAALAMU wa sekta Mifugo Tanzania wametakiwa kuongeza ushirikiano katika kujadili na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa ajili ya kuendelea kulijenga Taifa na kulipatia maendeleo endelevu kupitia sekta hiyo.
Akizungumza katika kikao cha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Tanzania Amosy Kulwa Zephania alisema, ushirikiano ni muhimu katika kulijenga na kuliendeleza Taifa kiuchumi.
Alisema kuwa, mifugo ni msingi mkuu katika kuliendeleza Taifa kiuchumi, hivyo ni wajibu wa wataalamu hao kukaa pamoja kutafuta namna bora itakayowasaidia wafugaji kunufaika na shughuli zao hizo.
“Ni muhimu sana kukutana na wataalamu katika kujadili jambo hili, kwani tunasaidia kuchangia sana maisha ya watu kutokana na kuwa mifugo inaweza kuwainua wananchi”, alisema Kaimu huyo.
Aidha alieleza kuwa, kuwepo kwa vikao hivyo kutaziwezesha wizara hizo mbili kupata utaalamu mpya wa kuweza kuinua sekta ya mifugo kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Maryam Abdalla Sadala alisema, mifugo na mazao yaliyopo yanawanufaisha wananchi wa Tanzania, hivyo wataendelea kushirikiana ili kuwa na uchumi jumishi kwa jamii yao.
“Ushirikiano huu tunaamini kwamba utazaa matunda, kwani tunakaa pamoja kubadilishana mawazo na kutafuta mbinu mbadala ya kuwasaidia wananchi wetu kutatua changamoto zinazowakabili ambazo tunazipendekeza kwenye vikao vyetu”, alisema Katibu Mkuu huyo.
Mapema Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo Pemba, Hakimu Vuai Shein alisema, kupitia vikao hivyo kutaondoa changamoto za kiutendaji, jambo ambalo litasaidia kupatikana mafanikio kwa wananchi.
Kikao hicho cha kubadilishana mawazo na kutatua changamoto ambazo wanazipendekeza katika vikao vya pamoja, kimefanyika katika Ukumbi wa Maktaba Chake Chake Pemba, ambao umewashirikisha Makatibu wakuu, wakurugenzi na watalamu wa sekta ya mifugo kutoka SMT na SMZ.