Wednesday, October 30

Timu ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Yakabidhiwa Vifaa Kwa Ajili ya Kushiriki Michuano ya Mabunge ya Afrika Afrika Mashariki.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi Seti ya jezi Mnazimu wa Baraza la Wawakilishi Mwakilishi wa Jimbo la Shauri Moyo Mhe.Hamza Hassan Juma, kwa ajili ya Timu ya Baraza inayotarajiwa kushiriki katika Michuano ya Mabunge ya Afrika Mashariki, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Baraza Chukwani Jijini Zanzibar.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikabidhiwa afano wa Hundi ya Shilingi Milioni Kumi na Tano na Uongozi wa Fumba Town Development kwa ajili ya Timu ya Baraza la Wawakilishi inayojiandaa na Michuano ya Mabunge ya Afrika Mashariki yanayofanyika Mkoani Arusha wiki ijayo.

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wachezaji wa timu za baraza la Wawakilishi wanaotarajia kushiriki katika mashindano ya mabunge Afrika Mashariki wakati alipokuwa akiwakabidhi vifaa kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo.

Na.Abdulrahim Khamis (OMPR)

Ushiriki wa timu ya Baraza la Wawakishi katika mashindano ya Mabunge ya Afrika Mashariki kutaisaidia kuitangaza Zanzibar kupitia sekta ya michezo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza  hayo wakati akikabidhi jezi pamoja na bendera ya Zanzibar kwa timu za Baraza la Wawakiishi zinazotarajiwa kushiriki michuano ya mabunge ya Afrika Mashariki, hafla iliyofanyika ukumbi wa Baraza la Wawakiishi Chukwan Jijini Zanzibar .

Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wananchi kwa ujumla wana imani na timu hizo, ambapo wanategemea ushindi katika michezo yote jambo ambalo litasaidia kukuza heshima ya Zanzibar kimichezo kimataifa ikiwa ndio shabaha ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kurudisha hadhi ya michezo nchini.

Alieleza kuwa ushiriki wa timu hizo ni mfano kwa wananchi wa Zanzibar kuwa na utayari wa kushiriki michezo kitaifa na kimataifa wakizingatia kuwa michezo ni afya pamoja na kukuza uhusiano na mataifa mbali mbali kikanda na kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka wanamichezo hao kuwa na uzalendo wanapokuwa katika mashindano hayo pamoja na kuzingatia sheria na nidhamu za kimichezo ili kuzijengea heshima timu hizo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru wadau mbali mbali waliosaidia timu hizo kupata nyenzo zote stahiki hadi kufikia sasa na kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuzungumza na wadau mbali mbali ili kusadiia kila mwaka timu hizo kuweza kushiriki katika michuano hiyo.

Nae, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid alisema timu hizo zimejiandaa vyema kushiriki katika michuano hiyo ambapo amemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa timu hizo zitarudi na ushindi kama ilivyoahidiwa.

Mhe. Zubeir alitumia nafasi hiyo kumshukuru Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungani wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kwa msaada wake alioutoa mpaka kufanikisha timu hiyo kukubaliwa ombi la kushiriki katika mashindano hayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa timu hiyo ambae pia ni Muwakiishi wa Jimbo la Shauri Moyo Mhe. Hamza Hassan Juma alisema kuwa nafasi hiyo ya kushirki katika michuano hiyo ni fursa ya kipekee ambayo Zanzibar iliomba kushiriki tokea mwaka 2005 ambapo kwa mwaka huu ni mara ya mwanzo kushiriki.

Aidha, Mhe. Hamza alimuomba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuandaa bajeti kwa kila mwaka kwa ajili ya michezo, ili kuweza kuwa na uhakika wa ushiriki wa michuano hiyo kwa pindi muda utakapowadia.

Katika makabidhiano hayo, kampuni ya Fumba Town Development ilikabidhi hundi ya shilling Millioni Kumi na Tano (15,000,000/=) ikiwa ni kuunga mkono timu hizo kwa ajili ya kushiriki katika mashindano hayo.

Timu za Baraza la Wawakilishi la Zanzibar zinategmea kuondoka nchini  Disemba 02, 2021 kuelekea Jijini Arusha kwa kushiriki michuano ya Mabunge ya Nchi za Afrika Mashariki  ambapo inajumuisha mashindano ya mchezo wa mpira wa miguu, na mpira wa kikapu kwa wanawake na wanaume.