\
NA HANIFA SALIM, PEMBA
WALIMU wa madrasa za Qur-ani Kisiwani Pemba wameishauri serikali endapo itambaini mwalimu wa madrasa kujihusisha na matendo ya udhalilishaji kumfungia na badala yake kumchukulia hatua kali ili kukomesha ambao wana tabia kama hizo.
Walisema, kuna baadhi ya walimu wa madrasa wamekua wakijihusisha na matendo ya udhalilishaji kwa wanafunzi wao jambo ambalo linawapotezea heshima walimu hao ndani ya jamii zao.
Waliyasema hayo wakitoa michango katika mafunzo hivi karibuni yaliyoandaliwa na ofisi ya mufti kupitia ofisi Rais katiba, sheria, utumishi wa umma na utawala bora yaliyofanyika ukumbi wa ofisi ya Rais fedha na mipango Gombani Chake chake.
Mjumbe wa jumuiya ya maendeleo Wilaya ya Wete Abubakar Hassan Suleiman, aliipongeza ofisi ya mufti ya kuwapatia mafunzo walimu hao ambayo itawawezesha kuwapatia leseni za kutambulika ndani ya serikali kwamba ni walimu wanaofaa.
“Naishukuru serikali kwa kuamua kwa makusudi mpango huu wa kutoa mafunzo kwa walimu wa madrasa ambao utasaidia sana maendeleo ya madrasa kwa umuhimu wa jambo hili nawanasihi walimu wenzangu tuitumie nafasi hii,” alisema.
Asya Mohamed Abrahman kutoka jumuiya ya wanawake wa Kiisilamu Pemba, aliomba ofisi ya mufti kuanzisha utaratibu wa kusomesha madrasa za Qur-ani kulingana na mbea mbili.
“Wanafunzi wanawake wasomeshwe na wanawake wenzao na wanaume wasomeshwe na wanaume wenzao na iwe ni sheria jambo hili litatuwezesha kufikia malengo katika suala zima la kupambana na udhalilishaji ndani ya jamii,” alisema.
Hata hiyo aliomba serikali kuwaunga mkono walimu wa madrasa kwa kuwawezesha kujipatia kipato kupitia wafadhili na viongozi mbali mbali wa taasisi na mashirika ili waweze kupata utulivu wakati wa ufundishaji.
“Pia iwekwe sheria Zanzibar kuwe na utaratibu wa mwanafunzi kujiunga na madrasa ajaze na fomu maalumu na kiwango cha mtoto kujiunga kwani skuli mzazi analipia fedha nyingi lakini kwetu 500 ambayo ni mchango hailetwi,” alisema.
Nae Afisa Madrasa na vyuo vya Qur-ani kutoka wizara ya elimu na mafunzo ya amali Pemba Omar Hamad alisema, walimu wa madrasa wamekua wakionekana na hamu kubwa ya kufundisha wameamua kupigana jihadi kutokana na hilo kwa kujitoa lakini kumekua na changamoto zinazowakabili.
“Walimu wetu wamekosa taratibu na njia za kufundishia ofisi ya mufti ni vyema wakaanza mchakato wa kuzikagua madrasa kama mwalimu haufikia vigezo basi hawezi kupata leseni ya kufundishia baada ya kupatiwa mafunzo haya,” alisema.
Mjumbe wa Baraza la maulamaa Pemba Sheikh Khamis Salim aliipongeza ofisi ya mufti ya kuanzisha utaratibu wa kuwapatia mafunzo walimu wa madrasa na kuwataka walimu hao kuifanyia kazi elimu waliopewa.
Sharif Makame Thani kutoka jumiya ya maimamu Zanzibar JUMAZA alisema, ofisi ya mufti licha ya kuandaa mafunzo ya walimu hao lakini kuna haja ya kufanya ziara za kutembelea madrasa kuona mazingira ambayo walimu wanafundishia.