NA KHADIJA KOMBO –PEMBA
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mheshimiwa Salama Mbarouk Khatib amesema suala la kuimarisha utawala bora ni wajibu wa kila mmoja kwa nafasi yake kwa kutekeleza kwa Vitendo misingi ya Utawala bora ili kuimarisha maendeleo ya Zanzibar.
Akizungumza katika Kongamano la siku moja lililowashirikisha Wakuu wa Wilaya, MakatibuTawala, Maafisa wadhamini pamoja na Wakuu wa Taasisi mbali mbali Kisiwani Pemba , huko katika Ukumbi wa Hoteli ya Green Foliage Mgogoni Chake Chake ikiwa ni katika shamrashamra za kuelekea siku ya utawala bora amesema tokea mwaka 1964 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikiimarisha misingi ya utawala bora kwani ndio itakayosaidia kuleta maendeleo nchini.
Wakiwasilisha mada juu ya Utawala wa sheria katika kujenga jamii yenye kuwajibika Dk Said Khamis Juma na mada juu ya Uzalendo DR. Godfrey Emiliano Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam wamesema Utawala bora ni dhana ambayo ina mambo mengi ya msingi, ikiwemo uwajibikaji na Uzalendo hivyo hakuna budi kufuata misngi hiyo kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa Ujumla.
Kwa Upande wao washiriki wa Kongamano hilo wamesema msingi ya utawala bora inahitaji kujengwa kwa vitendo hivyo jamii nayo inahitaji kuelimishwa ili kujenga nguvu za pamoja katika kutekeleza dhana hio ili maendeleo ya haraka yaweze kupatikana.
Jumla ya mada nne ziliwasilishwa katika Kongamano hilo ikiwa ni pamoja na Mgongano wa Kimaslahi ,Umuhimu wa utawala bora katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar, Utawala wa sheria katika jamii yenye kuwajibika, pamoja na uzalendo .
KUANGALIA VIDEO BOFYA HAPO CHINI.