Sunday, November 24

WANAWAKE Pemba wataja changamoto wanzokumbana nazo kufikia uongozi ndani ya siku 16 za kupinga udhalilishaji.

 

NA ABDI SULEIMAN

WAKATI Mataifa mbali mbali yakiungana Duniani, katika siku 16 za kupiga ukatili wa kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto, Tanzania ni miongioni mwa nchi zinaendelea na kampeni hiyo kila mwaka.

Niwazi bado matukio ya udhalilishaji, yamekua ni changamoto kubwa katika jamii hali inayopelekea kukata tama kwa wanaharakati.

Siku hii ilianzishwa mwaka 1991 ikiongozwa na kituo cha kimataifa cha wanawake, Zanzibar nayo inaungana na watanzania katika kuadhimisha siku hiyo, ikiwemo makongamano, mikutano, warsha za vijana, wanafunzi na midahalo ya watoto na watu wazima.

Makala haya imeangalia changamoto au vikwazo wanavyokumbana navyo wanawake, wanapoingia katika masuala ya uongozi katika nafasi mbali mbali.

Changamoto hizo ni pamoja na Rushwa, imani potofu kwa wanawake, ukosefu wa elimu na uwelewa mdogo kwao imekuwa ni kikwazo cha kukwamisha ndoto zao kuingia kuwania uongozi.

NI VIKWAZO VIPI WANAVYOKUMBANA NAVYO WANAWAKe

Asha Khamis Juma mkaazi wa Wingwi Wilaya ya Micheweni, suala la Rushwa imekuwa ni kikwazo kikubwa kinachokwamisha juhudi za wanawake, kuingia katika masuala ya uongozi katika kipindi cha Uchaguzi.

Anasema uwezo mdogo wa wanawake ikilinganishwa na wanaume au baadhi ya wagombea, ambao wanawania kipindi chengine katika jimbo kutokana na kutumika kwa fedha nyingi kwao.

Anasema “Utamuona mjumbe anakwambia wazi wazi wewe kaa tu wenzako wanatembeza bahasha, ukitizama wewe huna kitu na kazi kubwa umeshaifanya kwa wajumbe, mwisho wake tunaanguka katika kura za maoni na hata jimboni”.

Mtumwa Hassan Mwalimu mkaazi wa Wingwi, anesema tatizo jengine ni Wivu kwa waume zao kudai, mwanamke akishapata uongozi sio mke tena na kushindwa kuwa na muda wa kuhudumia familia yake.

“Hizi ni imani potofu kwa baadhi ya wanaume kushindwa kuwaruhusu na kuwaamini wake zao, kisingizio watakuwa sio wake zao tena jambo linalowakosesha haki zao”alisema.

Time Khamis Juma anasema kikwazo chengine ni ukosefu wa elimu kwa wanawake wa vijijini, kushindwa kufikia malengo ya kugombania nafasi za uongozi.

Wapo baadhi ya wanawake hujitokeza kugombani nafasi za uongozi ndani ya vikundi vya ushirika, vyama vya siasa hata katika kamati za maendeleo, lakini hushindwa kujieleza kwao hupelekea kukosa nafasi hizo.

Naye mkaazi wa Uwandani Siti Othaman, anasema tatizo ni mfumo dume uliopo katika jamii, mwanamke hawezi kufanya lolote mpaka apate ruhusa kutoka kwa mume wake.

Hata hivyo Halima Ali Othaman Mkaazi wa Uwandani, amewataka wanawake wenzake kuhakikisha wanazitumia fursa hizo zinapotoka, na sio kuwaachia wanaume kwani dunia sasa imebadilika.

JEE!!! WANAUME NAO WANASEMAJE JUU YA WANAWAKE.

Ali Mohamed Bakari mkaazi wa Tumbe, anasema ukosefu wa rasilimali Fedha kwa wanawake pamoja na mifumo ya uongozi iliyopo, inakwamisha mwanawake kugombania katika ngazi mbali mbali.

Wakati umefika kwa wanawake kujitambua kama wanaushawishi mkubwa katika jamii, hivyo wanapaswa kusimama kidete kuwania nafasi za uongozi nchini.

“Toka asubuhi mwanamke kuzungumza mbele ya wanaume inakua ngumu, lazima tuwaandae katika kuzungumza, kujiamini hapo ndipo tutaweza kuwapata wanawake shupavu wakushindana na wanaume majimboni”amesema.

Kombo Ali Abdalla (Mbunge) Mkaazi wa Uwandani, amesema bado nafasi ya mwanamke ni ndogo katika kuwania Uongozi, kutokana kuwa wanawake wengi kutokuwa na uwezo wa kufikia maelengo.

“Sababu inayowakwamisha ni kutokua na elimu katika masusalama mazima ya Uongozi, PEGAO munapopaswa kupakamata hapa lazima wanawake wajengewe uwezo zaidi huku vijijini”amesema.

Naye Aboubakar Juma mkaazi wa ndagoni, amesema tatizo jengine ni waume zao kuwazuwia kutokana na wivu walionao, na kuona mwanamke atabadilika baada ya kupata nafasi hiyo.

Mohamed Mbarouk Mohamed mkaazi wa ndagoni, amesema dunia ya sasa sio ya kutegemea mtu mwengine, vizuri kila mtu kuhangaika katika utafutaji wa huduma, hivyo ni wazi wanawake kujitokeza kugombania nafasi za uongozi.

“Ndagoni wanawake wapo tayari kugombania katika uongozi elimu ndio kikwazo kikubwa kwao, kinachopelekea kurudisha nyuma jitihada zao”alisema.

Naye Shaban Juma Kassim mkaazi wa shehia ya Makombeni, amewasihi wanawake wanapotaka kugombania kuhakikisha wanashirikiana pamoja na kuwa na sauti moja katika majimbo yao, ili kuweza kupata viongozi bora.

“Watakaposhirikiana na kuwa kitu kimoja, kutokana na wingi wao basi hakuna hata mwanamme mmoja atakaeweza kushinda ikizingatiwa wapiga kura wengi ni wanawake”amesema.

WANAWAKE WALIOKOSA NAFASI ZA UONGOZI WANASEMAJE

Salma Khamis Juma amesema tama kwa wanawake wenzake ndio iliyopelekea kukosa nafasi katika uchaguzi wa 2020, huku akiwataka viongozi kuhakikisha wanawapa nafasi kubwa wanawake katika masuala ya uongozi.

“Mimi binfasi nilikuwa bado kura moja tu kuwa mshindi katika kura za jimboni, alitoka mwanamke mwenzaku awambia mmoja ya mjumbe usimpe kura huyo mpe Fulani, ndio ikawa kura ya mwisho kuikosa na niishara kuwa hatupendani sisi wanawake tunahiyari mwanamme”alisema.

Amesema tokea kutokea kwa tukio hilo mpaka leo, huyo mwanamke amekuwa akijuta kwa kitendo chake hicho kwani huyo kiongozi waliompakura ameshindwa kuwatimizia yale aliyoaahidi katika kampeni zake.

Naye Hadia Omar Dadi mkaazi wa Wingwi, amesema waume zao ndio kikwazo kikubwa kwao kwa kudai kuogopa kuwatoa Vikoa wake zao, hali inayopelekea kushindwa kuwarusu kugoambania nafasi za uongozi.

“Mimi binafsi nimeshagombania ubunge mara mbili ndani ya vipindi vitatu, 2020 nimeingia katika viti maalumu lakini hali imekua ngumu kwangu zaidi inapokuja suala la fedha na wala sijakata tama”amefahamisha.

Zuhura Mgeni Othman mkaazi wa Gombani, anasema changamoto kubwa inayowakamisha wanawake ni wanawake wenyewe kutokupendana, kuvunjana moyo kwa kutoleana maneno yasiofaa, ukosefu wa fedha wanapotaka kuingia majimboni, rushwa kwa baadhi ya wanasiasa wakubwa kwa wenzao wadogo.

WANAHAMISHAJI JAMII NAO WANASEMAJE

Ali Othaman Ali mhamasishaji jamii kutoka PEGAO, anasema hali inasikitisha kwa wanawake wanapoingia katika kuwania nafasi za uongozi, huku akitolea mfano mwanamke mmoja katika jimbo la Wingwi alishindana na wanaume saba.

Amesema mwanamke huyo alikumbana na changamoto nyingi, hali iliyopelekea kukosa nafasi ya uongozi kutokana na kuwa pekee bila ya kuungwa mkono na wanawake wenzake.

“Niwakati sasa wanawake kumuunga mkono mwanamke mwenzo, wakati anapoamua kugombania nafasi za uongozi na sio kuwaunga mkono wanaume”amesema.

Naye Ali Abdalla Hamad, anasema wanawake wanapaswa kuwa imara kuwania nafasi za uongozi katika ngazi zote, ikiwemo siasa, NGOs na hata katika shehia.

Muhamasishaji mwengine Safia Saleh Sultani, amesema uongozi hauko katika siasa tu bali uko katika Nyanja mbali mbali, ikiwemo vikundi vya ushirika, wanawake kuwa mstari wa mbele katika kugombania nafasi za uongozi, na kuwataka akinababa kuacha kuwapa vikwazo wake zao wakati wanapotaka kugombania.

Kwa upande mwengine Siti Habibu, amesema umri sio kikwazo kwa mwananmke kushindwa kugiombania nafasi za uongozi, bali anapaswa kuwa shupavu na mstari wa mbele kutambua nini anachikitaka kwa jamii.

WANAHARAKATI NAO WANAYAPI YA KUSEMA

Mwenyekiti wa Jumuiya ya PEGAO Ali Mohamed Ali, amesema uongozi sio uhuni wala sio kupoteza maadili, hivyo amewataka wanaume kuondosha dhana potofu kuwa wanawake hawezi kuongoza.

“Tunapaswa kuwaandaa vijana wetu hivi sasa kuingia katika masuala ya uongozi, hapa tunaanzia maskulini wanawake kuwania nafasi huko ili akifika juu ni rahisi kwakwe kufikia malengo”amesema.

Bado wanawake wananafasi kubwa ya kuingia katika uongozi, huku akiwataka wanaume kuacha dhana potofu kuwa mwanamke akishapata ndio basi tena.

Mrtib wa TAMWA-zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hiya Mussa Said, amewataka wanawake kusimama kidete nafasi zinapotokea kuingia ulingoni, pamoja na kuachana na tabia ya kuvunjana moyo wanawake kwa wanawake.

Mratibu wa Mradi wa ushirikishaji wa wanawake katika uongozi Dina Juma, amesema lengo ni kuwafikia wanawake 6000 zanzibar (Unguja na Pemba), kuwajengea uwezo ili kudai haki zao za kiuchumi na kisiasa.

Aidha amewasihi wanawake kuitumia fursa iliyowekwa na serikali, ili kuongeza idadi ya viongozi katika ngazi za maamuzi na kufikia malengo ya meleniam ya kuwa na usawa wa kijinsi katika nyanja tofauti.

Mkurugenzi wa Jumuiya ya PEGAO Hafidhi Abdi Said, amewataka wanawake kuhakikisha wanaachana na dhana potofu kuwa viongozi wataweza kuwasaidia kwa kila kitu, kwani wanapopata huwakimbia na kutafuta maeneo mengine ya kuishi.

“Niwazi wanawake kuwachagua wanawake wenzao katika nafasi za uongozi, pale wanapoona wanagombania na wanaume ili malengo ya wanawake yaweze kufikiwa.

VIONGOZI WA SERIKALI WANAWAKE WANASEMAJE WAO

MKUU wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, amesema wakati umefika kwa wanaume kuwaunga mkono wanawake wanaojitokeza katika kugombani nafasi za uongozi, ili waweze kuibadilisha muono wa jamii katika harakati za kisiasa.

Wanawake wanuwezo mkubwa wa kuiunganisha jamii, katika nyanja mbali mbali za kimaendeleo na kutokana na uwaminifu wao katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Wanapojitokeza wanawake kuwania nafasi za uongozi katika Nyanja mbali mbali, wanapaswa kuungwa mkono na makundi yote kwani wanawake ni waaminifu kwenye jamii”amesema.

Aidha katibu Tawala Wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, amewahimiza wanawake kupendana wakati fursa za uongozi zinapotokea, ili wawe na sauti ya pamoja ya kuingia katika nafasi mbali mbali za kuiongoza jamii.

“Wanawake wenyewe wanashinda kupendana na kuwa kitu kimoja wakati nafasi za uongozi zinapotokea, hali inayopelekea kuwapa nafasi kubwa wanaume”amefahamisha.