Na Lulu Mussa -Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo leo tarehe 10 Disemba, 2021 amekabidhi Mpango Kazi wa Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira na Mwongozo wa Tuzo ya Taifa ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira kwa wajumbe wa Kamati Maalumu ya Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira katika kikao kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Mohammed Khamis Abdulla, amesema Lengo la Kampeni hiyo ni kuelimisha na kuhamasisha ushiriki wa jamii na uwajibikaji wa mamlaka za usimamizi katika hifadhi na usafi wa mazingira ili kuleta ustawi wa jamii ya watanzania na maendeleo endelevu.
Katika kufanikisha utekelezaji wa Kampeni hiyo, Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa Mpango Kazi wa Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira wa Kipindi cha Miaka Mitano 2021-2026, Mwongozo wa Tuzo ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira na Rasimu ya Mkakati wa Kutafuta Fedha za kuwezesha utekelezaji wa Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira.
“Nyaraka hizi ni vitendea kazi vya Kamati hii Maalumu pamoja na jamii ya watanzania katika utekelezaji wa Kampeni hii. Hivyo ninawakabidhi rasmi nyaraka hizi muhimu kama ishara ya kuwa kazi imeanza rasmi. Niwaombe mtoe uzito wa pekee katika kutekeleza majukumu hayo ya hiari ili kuwezesha kufikiwa kwa lengo la Kampeni” Jafo alisisitiza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Kampeni Kabambe Bw. Seif Ally Seif amesema kwamba, ni imani yake kuwa utekelezaji wa Kampeni hiyo utaanza mara moja na kuwa Kamati yake iko tayari kuungana na Serikali katika kuwezesha utekelezaji wake kwa ufanisi mkubwa.
Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira ilizinduliwa tarehe 5 Juni, 2021 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani na Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kampeni hii itakuwa endelevu na itatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2026.
Wajumbe hawa wa Kamati Maalumu wanatoka katika taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Sekta Binafsi, Serikali Kuu, Mashirika ya Umma, Mashirika ya Kimataifa, Asasi Zisizo za Kiserikali, na Taasisi za Fedha.