Thursday, January 16

DC Chake ameitaka KAMATI ya utalii kuibua, kufuatilia na kusimamia vyanzo vipya vya kiutalii ndani ya wilaya zao.

NA HANIFA SALIM, PEMBA

KAMATI ya utalii ya Wilaya ya Chake chake imetakiwa kuibua, kufuatilia na kusimamia vyanzo vipya vya kiutalii, katika maeneo yao ili kukuza sekta hiyo ndani ya Kisiwa cha Pemba.

Mkuu wa Wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali, aliyasema hayo alipokua akifungua semina ya siku moja kwa wanakamati hao katika ukumbi wa ofisi yake, na kuwataka kuvifikia vyanzo vipya vya utalii, ili serikali iweze kufaidika na vyanzo hivyo.

Alisema kuwa vipo vyanzo vingi ndani ya Wilaya ya Chake chake havijafikiwa, hivyo aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kuweka mipango mizuri ya kuitumia fursa hiyo, ili Wilaya hiyo iweze kupiga hatua kupitia sekta ya utalii ndani ya Kisiwa hicho.

“Lazima tuwe wabunifu, tuwe wajanja katika kukuza sekta ya utalii ndani ya Kisiwani cha Pemba sisi kamati lazima tuibue, tusimamie, na kuwashajihisha wenzetu kwa ajili ya kuboresha sekta hii, vyanzo vingi vimejificha na sisi tunaviona ni vyakawaida lakini ni vitu vya kuvutia kwa wageni”, alisema.

Aidha alisema, mtalii yoyote anaetoka nje ya nchi anahitaji suala zima la usalama wa kiafya, kimwili, chakula na mengineyo hivyo, aliisisitiza kamati hiyo kuwa wao ndio ngazi ya kuweza kuhuwisha utalii ndani ya maeneo yao.

Mapema Mdhamini wa Kamisheni ya Utalii Pemba Hamad Amini alisema, lengo la kuundwa kwa kamati hizo ni kuibua mambo mengi yanayoweza kuikuza sekta ya utalii nchini.

Alisema kuwa, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza shughuli za utalii imeona ipo haja ya kuziunda kamati hizo kwa Unguja na Pemba ili kuimarisha sekta hiyo.

Akiwasilisha mada ya mchango wa kamati za utalii katika kuimarisha uchumi wa buluu Zanzibar Afisa utalii Mkoa wa Kaskazini Swaleh Malik Abdi alisema, kamati hizo zimeundwa kwa lengo la kuupeleka utalii katika ngazi za chini kutoka serikali kuu kumpatia fursa kila mwananchi kutoa mchango wake.

Alisema, majukumu ya kamati hizo ni kuimarisha dhana ya utalii kwa wote, kudhibiti usalama na amani kwa wageni na jamii kwenye maeneo ya utalii, kulinda tamaduni za kiasili za Zanzibar, kuimarisha ubora na thamani kwa bidhaa za asili na kudhibiti thamani ya maadili katika jamii.

Akiwasilisha mada ya mitego ya utalii kupitia kamati za Wilaya Afisa utalii Mkoa wa Kusini Mohamed Ali Juma alisema,  kwa muda mrefu Pemba imekosa mpangilio bora wa huduma na shughuli za kitalii na si kwa sababu hazipo ila mapungufu katika miondombinu yake.

Kwa upande wao wajumbe wa kamati hiyo walisema jamii bado haina uwelewa juu ya suala zima la utalii hivyo, waliishauri wizara kuandaa mpango wa kutoa elimu kwa shehia sambamba na kuimarisha vivutio vya utalii ili wageni waweze kushajihika na utalii wa Kisiwa cha Pemba.