Thursday, January 16

RC Mattar amewasihi Mahakimu na Majaji Kisiwani Pemba, kutumia taaluma zao kwa kufanya uwadilifu na kuzingatia misingi ya haki.

NA ABDI SULEIMAN.

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, amewasihi Mahakimu na Majaji Kisiwani Pemba, kutumia taaluma zao kwa kufanya uwadilifu kwa kuzingatia misingi ya haki, bila ya woga wala upendeleo na kufuata sheria ili kuwajengea imani wananchi na mahakama.

Alisema uwamuzi wa Hakimu na Jaji unagusa uhai, mali na hali ya mwanadamu mwengine na watanzania, hivyo kosa lolote la kimaamuzi utakalotoa siku ya kwanza ya uhakimu na siku zijazo, litakua na faida au hasara kwa nchi, watu na familia.

Mkuu huyo wa Mkoa aliyaeleza hayo wakati akifungua mafunzo ya mahakimu juu ya upatikanaji wa haki kwa watu wasiokua na uwezo na wenye mahitaji maalumu katika mahakama, nakutolewa na idara ya katiba na msaada wa kisheria Zanzibar kwa kushirikiana na taasisi ya LSF na kufanyika mjini Chake Chake.

“Hatutegemei mahakimu kufanya makosa katika maeneo ambayo sheria iko wazi, kwa sababu hakimu anatakiwa kujitayarisha sana zipo kanuni na maadili zinasisitiza mahakimu na watumishi wa mahakama hawako juu ya sheria na wamewekewa mifumo ya uwajibikaji”alisema.

Aidha aliwataka kutokukubali kuendeleza vishawishi vya aina yoyote ile kitoka ndani ya mahakama au nje ya mahakama vitakavyojaribu kuingilia maamuzi yao.

Mkuu huyo alisikitisha na tabia za Mahakimu wengi kuhairisha kesi na sio kuzisikiliza, jambo ambalo sio utaratibu na bali wanapaswa kuzisilikiliza kwanza ndipo wazihairishe.

“Kazi za utoaji wa msaada wa kisheria zitasaidia sana wananchi kujua sheria na njia muwafaka za kuweza kuepukana na matendo ya makosa”alisema.

Hata hivyo alifahamisha kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa mahakimu na majaji, katika utoaji wa haki zaidi kwa kuzingatia watu wasio na uwezo na wenye mahitaji maalumu nchini.

Afisa mdhamini Ofisi ya Rais Katiba, katiba, sheria, utumishi wa umma na utawala bora Pemba Halima Khamis Ali, alisema kutolewa kwa mafunzo hayo ni mikakati ya Ofisi ya Rais Katiba sheria, kupitia idara ya msada wa kisheria.

Kwa upande wake Afisa miradi kutoka taasisi ya LSF Zanzibar Maryam Mansab, alisema kipaombele cha LSF ni kuboresha mashirikiano na serikali katika masuala mbali mbali ya kisheria na kutekeleza majukumu ya upatikanaji wa haki Zanzibar.

Alisema Matumaini ya LSF katika taasisi za kisheria, mafunzo hayo yataongeza ufanisi katika huduma za uotoaji haki kwa watu wasio kuwa na uwezo na watu wenye mahitaji maalumu nchini.

Naye Mkurugenzi wa idara ya utawala bora na kaimu mkurugenzi wa idara ya katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar Zaina Daudi Khalid, alisema mafunzo hayo yataweza kufungua ukurasa mpya katika kuhakikisha, mahakimu na watendaji wengine wa mahakama, wanawafikia wananchi wasiokuwa na uwezo na wenye mahitaji maalumu katika kuwapatia msaada wakisheria.

Alisema mafunzo hayo yataongeza mashirikiana baina ya watendaji wa mahakama na watoa msaada wakisheria, katika kuimarisha upatikanaji wa haki kwenye msaada wa kisheria.