NA ABDI SULEIMAN.
AFISA miradi ya Afya kutoka Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Zaria Haji Abasi, amewasihi madaktari kufanya kazi zao kwa bidii, kujituma na kujitambua katika ufanyaji wao wa kazi kwa lengo la kuwatumika wananchi.
Alisema kazi ya udaktari ni kazi ya kujitolea, hivyo wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa kufuata maadili na miko ya udaktari, ili kuona lengo linafikiwa.
Afisa huyo aliyaeleza hayo wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari, wakati wa ziara maalumu ya mashirikiano kutoka katika vituo 12 vya afya ambavyo vimo katika shehia zilizomo ndani ya mradi ya miradi ya milele, huko kituo cha afya Pujini.
Alisema lengo ni kujifunza na kuona unanyaji kazi wa madaktari wenzako wenzao, ili kwenda kuyafanyia kazi katika vituo vyao vya afya.
Aidha alisema madkatari wa kituo cha afya Pujini ni kituo cha mfano kwani madaktari wanafanya kazi kwa umoja mshikamano na kiko safi, hivyo changamoto ndogondogo haziwezi kuepukika.
Afisa afya Wilaya ya Chake Chake Mohamed Ali Jape, alisema kuongezeka kwa wagonjwa katika kituo hicho, imetokana baadhi ya vituo kuwa mbali kama vile Chambani au kiwani, hivyo wananchi wengi hukitumia kituo cha Pujini kupata matibabu.
Aidha aliahidi changamoto zilizojitokeza katika kituo hicho, wata hakikisha wanazifanyia kazi ili kuendeleza umoja na mshikamano wao katika utoaji wa huduma.
Aidha aliitaka Milele katika mradi unaokuja 2022 kuhakikisha wanaboresha zaidi baadhi ya vituo, katika suala zima la utoaji wa huduma na kuongeza vifaa vya kisasa.
Kwa upande wake Dr.Nassra Abdalla Juma,alisema kituo chao kwa wiki kinatoa huduma kwa wananchi 60 hadi 80 na kwa mwezi wanafika wagonjwa 600 hadi 800, na kutoa huduma mbali mbali ikiwemo chanjo, upimaji wa damu.
Aidha alisema wazazi 39 hujifunguliwa kituoni hapo kwa mwezi, ikizingatiwa ni idadi kubwa ya wananchi ndani ya kituo hicho wanapata huduma.
Akizungumzia Changamoto alisema ni ukosefu wa wasaidia ambapo waliopo ni nane, ukosefu wa baadhi ya vifaa muhimu katika hospitali hiyo ikiwemo vya kupimia, kuchunguzia maradhi mbali mbali.
Naye Yussuf Hamad Rashid daktari wa maabara, aliiyomba Milele kuwajengea maabara ya kisasa, ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi, ikizingatiwa kituo hicho kimekua ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa vijijini.
Siti Mohamed Massoud daktari kutoka kituo cha afya Kengeja, alisema kituo cha afya Pujini wanajitahidi katika utunzaji na utoaji wao wa huduma kwa wananchi.
“Tulitegemea kituoni hapa kuona watu watalalamika kutokana na sisi tunaingia huku na huku na wao wanahitaji huduma, ila kutokana na umahiri wa madaktari wananchi wametulia”alisema.
Afisa utabibu kutoka Micheweni Sharif sheha Hamad, aliwataka madaktari wenzake, kuhakikisha wanayafanyia kazi ipasavyo mema yote waliojifunza katika kituo cha afya Pujini.