Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika kipindi cha miaka 58 tokea kufuzu kwa Mapinduzi yaliyoongozwa na Waasisi chini ya Jemedari wa Mapinduzi Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Rais Dk. Mwiyi aliyasema hayo leo katika uzinduzi wa Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), ya kuadhimisha miaka 58 ya shamrashamra za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na mwaka 1964.
Katika hotuba yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa muasisi huyo wa Mapinduzi pamoja na wazalendo wenzake walijitoa muhanga kuikomboa Zanzibar hivyo ji wajibu wa watu wote kuendeleza pale walipofikia wao kwa faida ya kizazi hiki na cha baadae.
Alisema kuwa amevutiwa na kuandaliwa kwa utaratibu huo wa kuwajumuisha vijana kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na kuwa pamoja katika masuala ya kuhamasishana uzalendo na umoja juu ya masuala muhimu yanayohusu mustakabali wa Taifa hili likiwemo suala la kuyadumisha, kuyaendeleza na kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 yaliyoleta Uhuru wa kweli wa wananchinwa Zanzibar.
Aliongeza kuwa ni wajibu ya watu wote kuyaldumisha na kuendeleza matunda ya Mapinduzi katika kuimarisha uchumi kwa kuwezesha hali ya kipato cha wananchi na ustawi wao uendelee kuwa bora zaidi.
Alisema kuwa ujenzi wa uchumi wa kisasa unaodhamiriwa kujengwa .
Wajibu wetu sote ni kuyadumisha na kuendeleza matunda ya Mapinduzi katika kuimarisha uchumi kwa kuwezesha hali ya kipato cha wananchi na ustawi wao uendelee kuwa bora zaidi. Kwa hivyo, ujenzi wa uchumi wa kisasa tunaodhamiria kuujenga una lengo la kuziendeleza jitihada na mafanikio ya awamu za uongozi zilizotangulia na kuelekeza nguvu katika kuleta Mapinduzi ya Kiuchumi. Napata faraja kuona kuwa licha ya changamoto zilizotokana na athari za UVIKO – 19, tumeanza kupiga hatua taratibu kwenda kule tulikokudhamiria. Hivyo ni wajibu wa wananchi wote kuunga mkono na kushirikiana na Serikali katika kuyafikia malengo yetu ya kuwatumikia na kukabiliana na changamoto zilizopo.
Ni dhahiri kuwa uwajibikaji, uzalendo na mashirikiano kati yetu ni mambo ya msingi yatakayotuwezesha kupiga hatua zaidi za maendeleo na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazotukabili zikiwemo tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini kama ilivyo katika mataifa mengine.
Ndugu Viongozi na Washiriki wa Matembezi,
Kama ilivyo kwa Serikali za Awamu zilizotangulia, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane inalizingatia kundi la vijana kuwa ni kundi maalum lenye changamoto ambazo ni wajibu wa Serikali kuzitafutia ufumbuzi.
Jitihada za Serikali zinazoendelea ni pamoja na kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa katika ngazi mbali mbali za elimu pamoja na kuboresha mafunzo ya ufundi wa fani mbalimbali kwa vijana wanaojiunga katika vyuo vya mafunzo ya amali. Hatua nyengine ni kuwahamasisha vijana kujiunga na Mabaraza ya vijana yaliyoanzishwa katika Wilaya zote Unguja na Pemba. Mabaraza ambayo shughuli zake zinasimamiwa na kuratibiwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Lengo la Serikali ni kuona kuwa mabaraza hayo yanakuwa ni majukwaa ya kuwaunganisha vijana, kuwawezesha kubuni miradi ya kiuchumi na kuwaendeleza kwa kuwapatia mitaji, vifaa, taaluma na masoko ya kuuzia bidhaa zao. Tuna matumaini makubwa kuwa mabaraza ya vijana yakiimarishwa vyema yatawasaidia sana vijana kukabiliana na tatizo la ajira.
Vile vile, Serikali kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao unafanyiwa marekebisho ili uweze kutoa huduma zake kwa ufanisi zaidi, unatoa msukumo maalumu kuwasaidia vijana hasa walioko kwenye vikundi kupata mikopo nafuu ya kuendesha shughuli zao zikiwemo za ujasiriamali. Kadhalika, katika fungu la fedha zilizotengwa na Serikali katika kuchochea kuondokana na mdodoro wa Uchumi, tumeona pana fursa nyingi za vijana wanaojihusisha na shughuli mbali mbali kuweza kunufaika na fedha hizo.
Kwa hivyo, ni vyema vijana mkaendelea kujipanga na kuona namna mtakavyoweza kunufaika na fursa mbali mbali za kujiajiri na kujipatia kipato kwa kuzingatia uchache wa fursa za ajira zinazopatikana Serikalini.
Ndugu Viongozi na Washiriki wa Matembezi,
Natumia fursa hii kuwakumbusha vijana kuwa nyinyi ndio tegemeo la nguvu kazi ya Taifa. Kwa hivyo, mna wajibu wa kujilinda katika kujiingiza kwenye mambo yote yanayoweza kuharibu maisha yenu yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya, vitendo vya udhalilishaji, vitendo vinavyoweza kusababisha maambukizi ya virusi vya UKIMWI pamoja na vitendo vinavyoweza kupelekea uvunjifu wa amani na mambo yote ya kuvunja sheria.
Ni wajibu wenu kuendelea kuwa wazalendo, wachapakazi, watetezi wa amani, umoja na mshikamano na walinzi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Muungano wa Tanzania kwa nguvu zenu zote. Kutokana na sifa hizo, mtaendelea kuwa hazina muhimu, tegemeo na Chem chem ya kupata viongozi wazalendo wa kuitumikia nchi yetu kwa dhamira ile ile ya Waasisi wa Taifa letu Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Ndugu Viongozi na Washiriki wa Matembezi,
Namalizia hotuba yangu kwa kutoa shukrani zangu tena kwa kualikwa kuja kuyazindua Matembezi haya ya vijana katika Maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi. Nakupongezeni sana washiriki nyote na kukutakieni kila la kheri ili muweze kukamilisha matembezi haya kama ilivyopangwa.
Nachukua fursa hii kuwashukuru watu wote waliyoyachangia na kuwezesha kufanikiwa kwa matayarisho ya Matembezi haya ya mwaka huu wa 2022.
Baada ya kusema hayo, sasa napenda nitangaze kuwa Matembezi ya Vijana katika Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar, yamezinduliwa rasmi.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari
Ikulu Zanzibar.