NA ABDI SULEIMAN.
KAMISHENI ya Utalii Pemba, imemtaka msimamizi wa ujenzi wa Planet Xancara Island Retreat katika kisiwa cha Shamiani Mwambe Wilaya ya Mkoani, kuhakikisha wageni anaowapokea kuwa ni wamiliki wa mradi huo na sio watalii kama inavyoelezwa.
Wamesema kumekua na taarifa kuwa msimamizi huyo, hupokea wageni katika Uwanja wa ndege na kuwapeleka Kisiwani huko na kurudi jioni, wakati mradi huo ndio kwanza upo katika hatua za ujenzi.
Mdhamini wa Kamisheni ya Utalii Pemba Hamadi Amini Ali, alisema baada ya kusikia taarifa hizo kamisheni imelazimika kufika kisiwani huko na kujiridhisha hayo yanayoelezwa kiuhalisia.
“Kwa sasa hakikisha mgeni yoyote anaekwenda kumchukua ni meneja wako au wahandisi wa ujenzi katika mradi huu, sio mgeni mwengine vyenginevyo utajiweka katika mazingira magumu”alisema.
Akizungumzia suala la uhamasishaji ukataji wa leseni kwa mwaka 2022, pamoja na ukaguzi wa mazingira, vyumba na maeneo ya jikoni, alimtaka meneja wa hoteli ya Pemba Lodge Shamiani Mwambe Islanda, kuhakikisha anafuta taratibu zote na miongozo ya kamisheni ya utalii.
Alisema wamelazimika kufanya ukaguzi huo, kwani baadhi ya Hoteli hufanya udanganyifu katika ujazaji wa fomu ya tathmini na ukataji wa leseni za biashara zao.
Afisa Utalii Mkoa wa Kusini Pemba Mohamed Ali Juma, aliwataka mameneja hao kuhakikisha wanakua makini, wakweli pamoja na kufuata taratibu zote za kiutalii kwa wageni wanaowapokea katika hoteli zao.
Meneja wa Pemba Lodge shamiani Mwambe Massoud Ali Hamad, alisema serikali inapaswa kwenda kutangaza utalii wa Kisiwa cha Pemba, katika nchi mbali mbali duniani kama zinavyofanya baadhi ya nchi na kuvutiwa wageni na wawekezaji.
Alisema wageni wengi wanapokua katika hoteli yao hupendelea kuja kwa boti kutoka hoteli ya Nungwi, kuliko kupanda ndege kutokana na kuwa ndege ni gharama dola 120 kwa dakika 25 unguja Pemba.
“Kama kutakua na uwanja wa ndege moja kwa moja kutoka Unguja hadi Pemba, basi ingekuwa rahisi kwa wageni kufika ila kwa sasa wanaona ghali kwa dakika hizo,”alisema.
Naye meneja wa mradi wa Planet Xancara Island Retreat Shamiani Mwambe Ali Acheni, alisema kwa sasa wanaokuja kisiwani huko ni Meneja wa mradi huo na mafundi na sio wageni kwani mradi ndio upo katika hatua za awali ujenzi.
Alisema kwa sasa hakuna mgeni yoyote anayepokea hatolini hapo na kuwataka maafisa uwatalii kuendelea kumuanini kwa sasa yupo katika ujenzi wa mradi wake.