Wednesday, March 12

ZANZIBAR ya neema, haki na amani inawezekana.

 

Salum Vuai

MSANII wa muziki wa mwambao Bi. Zuhra Saleh wa Mombasa nchini Kenya, aliwahi kuimba wimbo uliopewa jina, ‘Nipende bado niko hai, ukinipenda nipo kaburini umelitupa pendo lako hewani’.

Mantiki ya wimbo huo ilikuwa kuonesha umuhimu wa waja kuoneshana mapenzi ya kweli wakiwa hai kwenye mgongo wa ardhi, kwani mtu akichukuliwa na mauti, kilio hakitakuwa na maana yoyote, kwani tayari anakuwa mfu asiyekuwa na hisia, wala uwezo wa kuona, kusikia, kushika na kufanya jambo lolote.

Nimependa kuutolea mfano wimbo huo, nikiunasibisha pia na umuhimu wa watu wanaokosana kusameheana na kuweka kando tofauti zao wangali hai ili nao waridhiwe na Muumba wao.

Ni ukweli usio shaka kwamba katika kuishi pamoja, binadamu hawaachi kukosana au kukwaruzana kwa sababu mbalimbali.

Lakini hawapaswi kuwekeana mafundo nyoyoni na kukataa kuombana msamaha ili waendelee kuishi vizuri wakielewa kuwa kukosea ni sehemu ya maumbile ya binadamu.

Na katika suala la kuendesha nchi hasa katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, nchi mbalimbali hasa za bara la Afrika, zimekuwa zikiishi kwenye misuguano isiyokwisha, huku viongozi na wananchi wengine wanaotaka kushika madaraka wakijikita kwenye mivutano mikubwa isiyojulikana mwisho wake.

Migogoro mingi hutokea zaidi nyakati za uchaguzi wa kutafuta viongozi wa kushika khatamu ambapo kila upande hutumia kila aina ya mbinu kumpiku mwenzake ili ushike dola.

Tukiiangalia historia ya nchi yetu Zanzibar, chaguzi zetu tangu kabla ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964, zimekuwa zikitawaliwa na sitafahamu inayoacha dosari kubwa kwa ustawi wa visiwa hivi, kwani wananchi hujikuta katika wakati mgumu hata kujengeana uhasama na chuki wakisahau kwamba wao ni  ndugu wa nchi moja.

Hata hivyo, jambo la kushukuru ni kuona kuwa, pamoja na mashaka yote yatokanayo na chaguzi, bado tunaweza kutumia busara kwa kukaa mezani na kutafuta njia bora za kuleta suluhu, hali inayoimarisha amani na utulivu uliodumu nchini kwa karne nyingi sasa.

Wananchi wengi wa Zanzibar wametiwa moyo sana na hatua iliyochukuliwa na Rais Dkt. Hussein Mwinyi kuuita upande wa Chama cha ACT Wazalendo kilichoshika nafasi ya pili kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba 2020 ili kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ambayo ipo kikatiba.

Kwa dhamira waliyoionesha viongozi wetu hao, ni wajibu nasi wananchi tuwaunge mkono kwani siasa za uhasama, chuki na ubaguzi hazina tija na zikiachiwa kushamiri, matumaini ya kupata maendeleo zitakuwa ndoto za Alinacha.

Wakati viongozi wetu wakuu wametanabahi kwamba siasa za chuki hazitupeleki kwenye nchi yenye neema tunayoitarajia, si jambo la kiungwana kutokezea watu miongoni mwetu kulalamika chini chini wakipinga jitihada zao ambazo kimsingi zimelenga kuitoa Zanzibar kwenye jinamizi la uchumi duni linalosababishwa na mifarakano isiyofika mwisho.

Si katika maelekezo ya vitabu vya dini kwa watu wa nchi moja tena wengi wao wakiwa wa imani sawa, kukubali kuzainiwa na shetani aliyeweka ahadi ya kuwatoa kwenye njia ya haki na kuwapeleka katika batili.

Kama bado wapo Wazanzibari wanaodhani kwmba nchi hii ni ya watu wa kundi fulani peke yao na wengine hawana chao, nawashauri waache fikra hizo potofu kwani wao wenyewe hawana mkataba na Mwenyezi Mungu wa kuishi milele katika dunia hii.

Kama tulivyoirithi nchi hii kutoka kwa wazee wetu ikiwa salama na yenye neema za kila aina, nasi tunuwie kuwaachia watoto na wajukuu wetu ikiwa tulivu na yenye matunda yanayotoja asali badala ya shubiri.

Hive  karibuni  Asasi  ya Waandishi wa Habari Pemba kwa Kushirikiana na  Shirika la Internews  wameanza  kampeni maalum  kupitia  waandishi wa habari na kuwakutanisha wadau pamoja kwa  lengo la kutathini na kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kuwa na mijadala  chanya ambayo  inaweza kuchochea jamii  hali ya mtengamano , amani na umoja . Kwa kupitia mikutano ya wadau,mafunzo kwa waandishi wa habari ,mijadala ya redio  pamoja na kampeni kwa kutumia mitandao  ya kijamii inaweza  kutoa fursa kwa wananchi  kujadili ni mikabala gani  ambayo  inaweza  kusaidia   hali hii. Ni hatua zipi zinapaswa kuchukuliwa na viongozi , vyama vya kisiasa ba wadau  ambayo inaweza kusaidia kuleta matokeo ya amani yanayofaa.

Tunaamini  kwamba hali hii inaweza kuleta umoja, mshikamano na  kuzaa  zao la haki kwa wananchi  ambazo  wanazihitaji

Nahitimisha kwa kuwafumbua macho wale ambao bado wana mafundo wafahamu kwamba, nchi hii ikikatika vipande vipande hakuna faida yoyote watakayoipata wao wala wengineo, zaidi itakuwa hasara na kutafuta pa kukimbilia ambako si rahisi kupavumbua.

Tumuombe Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki Zanzibar kwa kuitunza amani yetu, ili iwe nchi ya wengine kuikimbilia na sio ya kukimbiwa na kila mmoja wetu.

Zanzibar yenye amani, imani, neema, baraka, upendo na umoja inawezekana na ndio tumaini la wengi kwani sisi si watu tuliozoea vurugu na vita, na hata marehemu Siti Binti Saad aliimba, “Unguja (Zanzibar) ni njema atakaye aje”.

Ni wajibu na jukumu letu kuifanya iwe  njema kikweli sio kwa nyimbo za majukwaani tu.