Monday, November 25

Ufugaji wa ng’ombe wa kisasa unarudisha nyuma kutokana na changamoto mbali mbali-Mfugaji Ahmed Shaaban Salim.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

UKOSEFU wa madawa, vyakula, mbegu, soko na kufeli kwa mashine ya kupimia mifugo yao, kunarudisha nyuma maendeleo yao ya ufugaji wa ng’ombe wa kisasa.

Mfugaji Ahmed Shaaban Salim mkaazi wa Wete ambae anafuga ng’ombe wa maziwa katika kijiji cha Kinyasini alisema, kuwepo kwa changamoto hizo zinawafanya wakaribie kukata tamaa katika kuendelea harakati za ufugaji.

Alisema kuwa, kwa sasa ana ng’ombe watano wakiwemo wa maziwa wanne, ambapo ng’ombe mmoja anazalisha lita 22 hadi 33 kwa siku, ingawa kuna mambo ambayo yanamrudisha nyuma kila siku zinapoendelea.

Alisema kuwa, kutokana na kiwango hicho cha uzalishaji wa maziwa, kungekuwa na soko la uhakika, angejipatia fedha nyingi na kuimarika kipato chake.

“Changamoto ni nyingi ingawa nakabiliana nazo ila wakati mwengine nashindwa, ikiwa nitatatuliwa changamoto hizi nitaweza kusonga mbele zaidi kimaisha”, alisema.

Alieleza kuwa, kutokana na kutokuwepo kwa soko la uhakika inasababisha ng’ombe asiwalishe vizuri na hatimae kupungua kiwango cha uzalishaji wa maziwa.

Aidha alieleza kuwa, maabara zinafeli, jambo ambalo wanashindwa kwenda kupima mifugo yao, huku akikosa mbegu za kupandishia kwani ng’ombe wanakuwa na joto jingi.

“Nilianza na ng’ombe watatu mpaka nikafikia kumi, lakini kutokana na hali iliyopo nimebakiwa na ng’ombe watano tu, hivyo naiomba Serikali inisaidie kutatua changamoto hizi, ili niweze kufaidika mimi na jamii, kwani natoa ajira kwa vijana”, alisema.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Tanzania Amosy Kulwa Zephania alisema, ni fursa kubwa kwa wafugaji ambayo inaweza kumuinua kimaisha, hivyo watashirikiana katika kuhakikisha wanatatua changamoto mbali mbali, ikiwemo kuwaletea mbegu wafugaji wa Zanzibar.

“Kuna magonjwa mengi ambayo huwapata mifugo yetu, hivyo tutayapima kwa pamoja na tutayatibu, tumeona kwamba huku Zanzibar ng’ombe wengi wanakabiliwa na ugonjwa wa Kiwele, hivyo tutahakikisha tunayadhibiti”, alisema Kaimu huyo.

Aliwataka wafugaji hao wafuge kulingana na mazingira, ili mfugaji apate tija zaidi na aweze kujikwamua na maisha duni.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Maryam Abdalla Sadala akizungumzia kuhusu soko alisema, watahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza Zanzibar sambamba na kuweka uimarishaji wa hilo, katika kuhakikisha maziwa yanakuwa na soko na kuwanufaisha wafugaji.

Alisema kuwa, kuna milioni 40 za kimarekani kwa ajili ya mifugo, hivyo waliiahidi Serikali kwamba zile ajira walizioahidi nazo zitapatikana kupitia sekta ya ufugaji.