Monday, November 25

10 wamefariki dunia na wengine 15, waokolewa wakiwa hai.

MWANDISHI WETU, MKOANI.

JUMLA ya watu 10 wamefariki dunia na wengine 15, wakiokolewa wakiwa hai baada ya boti waliokuwa wakisafiria kuzama katika bandari ya Kisiwapanza Mkoa wa kusini Pemba.

Kwa mujibu wa taarifa iliopatikana kutoka kwa mkuu wa Wilaya ya Mkoani  Khatib Juma Mjaja , zinaeleza kwamba watu 9 walipatikana mapema tarehe 4/1/2022  na mmoja alipatikana muda wasaa 6 ,usiku na kufikisha idadi hiyo.

Hata hivyo mbali na kupatikana maiti hizo kuna watu 15 ambao waliokolewa wakiwa hai na kuruhusiwa kurudi majumbani kwao wakiwa na hali njema.

“ Tumebahatika kuwaokowa watu 15 wakiwa hai na maiti kumi za wasafiri hao ambao tayari walishakabidhiwa kwa jamaa zao kwa mazishi, ingawaje juhudi za uokozi zinaendelea,”alieleza.

Mjaja aliwataka wananchi ambao wanajamaa zao wanadhani waliingia kwenye boti hiyo na hawajawaona mpaka sasa waripoti katika vyombo husika ili kuendelea kutafutwa ili wajuilikane kuwa wako hai ama wamefariki.

Alisema Serikali ya Wilaya iko pamoja na wale wote waliokumbwa na msiba huo na inaona kuwa ni msiba wao wote hivyo aliwataka kuwa na subra katika kipindi hichi cha maombolezo.

Hata hivyo akizungumzia suala la Covid 19, aliwataka  wananchi kuendelea kuchukuwa tahadhari katika mikusanyiko kama hiyo inayotokea kwa kuvaa barkoa na kukaa masafa makubwa ili kunusuru maambukizi.

Alisema ni vyema pale mtu atakapojiona hali yake sio mzuri basi akimbilie kwenye vituo vya afya kwa kufanya uchunguzi wa kitaalamu ili kujielewa hali yake na kujikinga ili kuepusha maambukizo kwa wenzake.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa Afya wilaya ya Mkoani Pemba, Mohammed Faki Saleh alithibitisha kupokelewa kwa maiti kumi na watu wengine kumi na tano  wakiokolewa wakiwa hai.

Alisema  baada ya kupokelewa Hospitalini Abdalla Mzee kufanyiwa uchunguzi na kuruhusiwa kurejea majumbani kwao huku maiti zikikabidhiwa kwa jamaa zao kwa mazishi baada ya uchunguzi.

Aliwataja watu waliofariki kuwa ni Omar Machano (50), Rashid Hamad (30),Suleiman Hamad (32), Moh’d Soud , Nassor Issa Omar (34),Salim Juma Said (55).

Maiti nyengine ni Ali Makame Shehe, Shasha Khamis Abdalla,Hassan Mati Haji (22) na Idrisa Omar Aley.

Waliokolewa wakiwa hai aliwataja kuwa ni Hamad Omar Mselem, Bambi , Khamis Ali Khator,Khalifa Moh’d Abdalla,Khamis Yussuf Moh’d, Haji Muhamad , Omar Jibran , Ali Shehe Othman , Suleiman Jibran , Bakar Salim Jibran, Suleiman Juma Moh’d,Shaaban Ali Hamad,Suleiman Moh’d Khamis,Haji Moh’d Juma, Abdalla Kassim Moh’d.

Kwa upande wake Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa , Serikali za mitaa na Idara maalum za SMZ, Massoud Ali Mohamed aliwatak wananchi kuendelea kushirikina pamoja katika mambo hayo yanapotokea na kwamba Serikali iko pamoja na wao.

Alisema Serikali ilishitushwa sana baada ya kupokea taarifa hizo na ndio tokea ilipotokea ajali hiyo viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Shehia , Wilaya na mkoa iko pamoja na wananchi ili kuokowa maiti hizo na kuokowa wale watu waliookolewa wakiwa hai.

“ Sisi Serikali tuko pamoja na nyinyi na msiba huu ni wetu sote , na ndio tokea jana viongozi wa Serikali tunashirikiana nanyinyi katika hili , ispokuwa tunawaomba muendelee kushirikiana na muendelee kuwa na subra na sisi tuna pita kila pahala penye msiba kutowa ushirikiano wetu,”alisema.

Nae Kamanda wa KMKM Zanzibar Comodoo Msingiri alimuhakikishia Waziri Massoud kuwa wanatekeleza maagizo aliyowapatia ya kutaka kuongezwa nguvu ya uokozi na kwamba hilo limefanyika na tayari wameshapeleka wazamiaji 12 ambao wako baharini kuangalia kama kuna watu waliobakia wakiwa hai au kufariki.

“ Mheshimiwa waziri tumepokea agizo lako kwani sisi kazi yetu moja ni Uokozi na sasa hivi tumeongeza wazamiaji 12 wako chini ya bahari kwa ajili ya kujiridhisha kama kuna miili ya watu imebaki huko tuweze kuiokowa na tutakapomaliza tutakupatia taarifa rasmi na hata ikibidhi kulala baharini tutalala,”alieleza Msingiri.

Nae mkuu wa Uzamiaji kutoka kikosi cha KMKM Pemba, Kassim Hussein Saleh alisema, tokea jana majira ya saa kumi kulipotokea ajali hiyo na kunza kuzamia zoezi lilikwenda vizuri na hadi wanasitisha kulikuwa na maiti 9 walishaziopoa kwenye maji na waliohai zaidi ya watu 12 kwa jana .

Kassim , alieleza kuwa bahari haina utafauti katika shuhuli za uokoaji kutoka jana la leo ispokuwa jana walifanya kwa haraka lakini leo wamekwenda vizuri na wamezama lakini hawakuambulia kitu ispokuwa wanasubiri maagizo kutoka kwa waziri ili waende kutafuta sehemu za mito ya mbele ili kuona kama kuna mtu amezama.

“ Kwa sababu maji yanatembea inawezekana kuchukuliwa mwili kupelekwa mbele na hatimae kukifanya doria tunauona , ispokuwa hatuna uhakika wa watu waliokuwemo ndani ya boti ni wangapi kutokana na tuliokuwa tunaokoa ni watu wa aina tafauti kuna watu wa nje walitusaidia na wengine waliokolewa walipelekwa ng’ambo nyengine , na ushirikiano wao ndio uliotufikisha hapa tulipo,”alisema.

Mzamiaji kutoka Kisiwa Panza mkoani Pemba, Mustafa Haji Seif alisema walishirikiana na kikosi cha KMKM mara baada ya kupata taarifa hizo majira ya saa 10 za jioni na wakaweza kuokowa  watu hao waliozama ingawaje habari ilikuwa chafu kwani baadae kulivuma upepo.

Hata hivyo alisema siku ya leo wameanguka mara mbili lakini hawakuona mwili mwengine wa mtu aliefariki au aliehai pamoja na kwamba wamekuta simu ambayo hawajaifanyia uchunguzi mwenyewe nani.