Monday, November 25

ALIYEMLAZIMISHA SPIKA KUJIUZURU NI HUYU!

Na Abbas Mwalimu (0719258484).
Alhamisi tarehe 6 Januari, 2022.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Yustino  Ndugai ameandika barua  rasmi kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi kujiuzuru nafasi yake ya Spika wa Bunge.
Katika taarifa ya iliyotolewa kwenye ukurasa rasmi wa Bunge Spika Ndugai ameeleza na hapa ninamnukuu:
“Naomba kutoa taarifa kwa umma wa watanzania kuwa leo tarehe 06 Januari ,2022 nimeandika barua kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kujiuzuru nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uamuzi huu ni binafsi na hiari na nimeufanya kwa kuzingatia na kujali maslahi mapana zaidi ya taifa langu, serikali na chama changu cha CCM.” Mwisho wa kunukuu.
Kutokana na maelezo haya ya Spika kuna swali la msingi hapa la kujiuliza, ni nani amemlazimisha Spika kujiuzuru?
Ili kufahamu aliyemlazimisha Spika kujiuzuru kuna haja ya kuifahamu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasemaje, pia Sheria namba 13 ya mwaka 1995 ya Maadili ya Viongozi wa Umma bila ya kusahau Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Juni, 2020.
Kwa kutumia miongozo hiyo tutamtambua aliyemlazimisha Spika Ndugai kujiuzuru.
Tukitazama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 84 Ibara ndogo ya 7 kifungu (h) inaeleza kama ifuatavyo:
Spika atakoma kuwa Spika na ataacha kiti cha Spika litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo-
(h) ikiwa itathibitika kuwa mtu huyo amevunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;
Je Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inasemaje?
Tukitazama Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inaelekeza yafuatayo katika kifungu cha 6 na cha 8:
Kifungu cha 6 kinabainisha hatua zinazoweza kuchukuliwa pindi kunapotokea mgongano baina ya maslahi binafsi ya kiongozi wa umma dhidi ya maslahi ya umma.
Kifungu hiki kinaeleza kama ifuatavyo:
‘Kuhusu maslahi ya umma, mara wanapoteuliwa au kuchaguliwa na hata baadae, viongozi wa umma wapange mambo yao kwa namna ambayo itazuia kutokea kwa migongano halisi ya maslahi au kuwepo na uwezekano wa migongano au kuonekana kuwepo migongano, lakini endapo migongano ya namna hiyo itatokea kati ya maslahi binafsi ya kiongozi wa umma na ya kazi zake rasmi na majukumu yake, migongano itatatuliwa kwa manufaa ya maslahi ya umma.’
Swali la msingi hapa ni hili, maslahi ya umma ni yepi hayo?
Tukitazama Ibara ya 8 ibara ndogo ya Kwanza kifungu (b) cha  Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kinabainisha Maslahi ya Umma katika muktadha wa ustawi kama ifuatavyo:
(b) lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi;
Tafsiri ya ustawi wa wananchi kwa lugha nyingine ni maendeleo ya wananchi.
Kwa kuzingatia lengo hilo la kuleta maendeleo kwa wananchi Serikali hulazimika hata kukopa ili kutekeleza miradi kama SGR ambayo inaenda kuchechemua uchumi na kuifungua nchi kibiashara.
Kwa mantiki hiyo basi, huenda kwa kauli aliyowahi kutoa Spika kuhusu mikopo kwa namna fulani inatafsirika kama ingeweza kukinzana na maslahi ya umma ambayo ni maendeleo ya wananchi kwa mujibu wa Katiba.
Kwa muktadha huo na kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha Sheria namba 13 ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 inaweza kutafsiriwa kama ukikwaji wa maadili ya viongozi wa umma.
Kifungu hiki cha 8 kimebainisha hatua mbalimbali ambazo kiongozi wa umma anaweza kuchukuliwa kudhibiti ukiukwaji wa maadili ya uongozi  ikiwemo:
(e) kumshauri kiongozi kujiuzulu wadhifa unaohusu ukiukaji huo;
Lakini je ni nani aliyemshauri Spika Ndugai kujiuzuru?
Hili ndiyo swali lingine ambalo linafaa kujiuliza.
Jawabu la swali hili limebainishwa katika Ibara ya 63 ibara ndogo ya Pili ya Katiba ambayo inasema:
Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.
Sote tunakumbuka kuwa kabla ya uamuzi huu wa Spika tulishuhudia vipande mbalimbali vya maelezo ya wabunge wakimtaka Spika ajiuzuru huku Wabunge  wengine wakiahidi kupeleka hoja ya kumwondoa Spika madarakani kwa mujibu wa kifungu cha 158 (1) cha Kanuni za Kudumu za Bunge sambamba na ibara ya 84 ibara ndogo ya 7 kifungu (d) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Miongoni mwa Wabunge hao ni Job Lusinde maarufu kama Kibajaji na Mchungaji Josephat Gwajima wa Jimbo la Kawe.
Kwa mujibu wa Ibara hiyo ya 63 (2) ya Katiba  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sauti ya wabunge ni sauti ya wananchi kwa sababu Wabunge hao  wamechaguliwa na wananchi, hivyo waliomshauri kujiuzuru ni wananchi wa Tanzania  kupitia kwa Wawakilishi wao ambao ni wabunge.
Hivyo basi kwa kuzingatia ushauri huo wa wananchi na kutokana kuwepo na tishio la kumwondoa  madarakani ambalo  Wawakilishi wa wananchi walionesha nia hiyo, Mheshimiwa Spika amejiuzuru kwa mujibu wa kifungu cha 158 kifungu kidogo cha 6 cha Kanuni za Kudumu za Bunge ambacho kinabainisha wazi kwamba:
*’Spika anayetuhumiwa anaweza kujiuzulu nafasi yake kwa kutoa maelezo ya kujiuzuru kwake Bungeni kabla ya uamuzi juu ya hoja ya kumwondoa madarakani.’*
Tuhuma zipi? Tuhuma za kukwamisha maendeleo ya wananchi kama zilivyoelezwa kwenye Ibara ya 8 (b) kwa jina la ustawi.
Tukumbuke hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan siku alipopokea Ripoti ya Mpango wa Kwanza wa Maendeleo na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 Ikulu jijini Dar es Salaam alisema kuwa aliposema kidogo tu wananchi wakajibu.
Hivyo kutokana na kauli ile wananchi wameona kuwa labda alikiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na hivyo walimshauri ajiuzuru nae amefanya hivyo. Tukumbuke Mheshimiwa Spika mwenyewe aliwaomba radhi watanzania (wananchi) siku alipofanya Mkutano na Waandishi wa habari.
Kwa hivyo basi, kwa mujibu wa Katiba  wananchi ndiyo waliomchagiza  Mheshimiwa Spika Job Ndugai kujiuzuru na ndiyo maana hata taarifa yake inasema anaujulisha umma yaani wananchi.