Monday, November 25

WAZIRI wa Utalii Zanzibar awafariji wahanga wa kuangukiwa na kidungu Pujini

NA ABDI SULEIMAN

WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Lela Muhamed Mussa, amewafariji wananchi na wafanya kazi waliopata ajali ya kuangukiwa na Dungu katika siku ya Utalii duniani mwaka jana.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inaendelea kuwathamini na kuwajali wananchi hao, ili kuona wanarudi katika hali zao za kawaida.

Waziri Lela aliyasema hayo kwa nyakati tafauti, Pujini Dodo, kibaridi na katika ofisi ya kamisheni ya utalii Pemba, alipowafariji wafanyakazi waliopata na mtihani huo.

Alisema katika kuadhimisha miaka 58 ya Mapinduzi na Mwaka Mmoja wa Wizara hiyo, ameona vizuri kuwajulia hali na kuona maendeleo ya afya zao na kama wapo ambao bado basi Wizara iweze kuwasaidia.

“Mimi nimekuja kuwajuulia hali zenu, kuona maendeleo yenu na kama bado Wizara ifanye juhudi kuwahudumia, hili limetokea hakuna aliyetaraji ila ni mitihani mungu ameshapanga tu”alisema.

Aidha Waziri huyo alimtaka Bimaimu Mohamed Chumu, kurudi tena hospitali kwa ajili ya kuondoshwa piopio mguuni na kufanyiwa vipimo tena ili kuona maendeleo ya mguu wake.

Aidha aliwashukuru na kuwapa pole wananchi waliopatwa na mtihani huo pamoja na wafanyakazi wawili wa wizara yake, kutokana na hali zao kuendelea kuimarika siku hadi siku.

“kutokana na hali iliyo inaonyesha hali zianendelea kuimarika kila kukicha, ni jambo zuri linatia moyo hakuna alioamini kama mutakua hivi yote ni mipango ya mungu tunapaswa kumshukuru”alisema.

Akitoa neno shukurani kwa niaba ya majeruhi wa tukio hilo, afisa Mdhamini Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Pemba Zuhura Mgeni Othaman, alimshukuru waziri huyo kwa juhudi na mikakati yake katika kuona waathirika hao wanapona kabisa na kurudi katika hali zao za zamani.

Kwa pande wake Mahmoud Mohamed Abdalla, mmoja wa waathirika wa tukio hilo, alimshukuru waziri huyo kwa kufika na kuwaona na kuwajulia hali zao, kwani tokea mwanzo wa tukio wizara imekua msaada mkubwa kwao.

Naye Mchanga Amour Khamis mkaazi wa Pujini Dodo, alisema bado kifua, tumbo na kiuno vinaumuma, huku akitia chakula hakikai tumboni na kukitoa.

Mwathirika mwengine ni Maimuna Mohamed Chumu, alisema sababu iliyopelekea kutokulitoa piopio mguu mwake, ni kutokana na kukosekana kwa EXRAY ya magoti katika hospitali ya Wete, Chake Chake na Mkoani.

Naye Rabia Ali Amour alisema kwa sasa anafanya shukuli zake ndogo ndogo kikamilifu, wakati kabla ya hapo hali yake ilikuwa ni mtihani kufanya kila kitu.

MWISHO