NA ABDI SULEIMAN.
WAONGOZAJI watalii Zanzibar wametakiwa kuweka tarifa za Popo wa Pemba kwa kina katika mitandao yao, kama walivyoweka taarifa za kima punju walioko jonzani Unguja, kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vilivyomo ndani ya Kisiwa hicho.
Hayo yameelezwa na Mjumbe kutoka ZTO Haji Juma Ramadhani,wakati wa kiangalia Popo wa Pemba waliopo Kilimo Wilaya ya Chake Chake, wakati wa ziara ya Mapinduzi Domestic Tour Zanzibar, iliyowashirikisha waongozaji watalii na waandishi wa habari.
Alisema wageni wengi wanapofika Unguja wanajua tayari wameshatembelea Zanzibar, kutokana na kuvutiwa kwao na taarifa zinazowekwa katika mitandao hiyo na kusahau kama Pemba nako kuna vivutio tena vizuri.
Alifahamisha kuwa Pemba kunavivutio vingi ambavyo havijatangazwa, hivyo niwakati sasa waongozaji wataalii kutumia fursa hiyo ya kuvitangaza ili kisiwa cha Pemba nacho kiweze kubadilika kiutalii.
Naye Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Lela Mohamed Mussa, alisema lengo la ziara hiyo kwa waongozaji watalii Unguja ni kutangaza vivutio vya utalii, ili kujenga uwelewa juu ya utalii, pamoja na kuongeza ushawishi wao.
Alisema kisiwa cha Pemba ni sehemu ya Mkakati katika uwekezaji, kwani mikakati ya serikali kujenga uwanja wa ndege wa kisasa ili ndege kubwa ziweze kutua, bandari ya mkoani kupokea meli kubwa kama ilivyo bandari ya unguja.
Aidha alitaka wananchi kufahamu kuwa utalii wa Pemba hautokua utalii rahisi, hoteli zote zitakzojengwa Pemba zitakuwa za nyota tano na zenye hadhi kubwa, kwa ajili ya wageni kama ilivyo mikakati ya serikali.
“Serikali imeamua kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa ni kisiwa cha mkakati katika uwekezaji, hoteli zote zitakazojengwa zitakua sawa, wananchi kujipanga kupokea utalii huo kwani hautokua na madhara kwao,”alisema.
Aidha aliwataka wananchi, taasisi binafsi na mashirika kushirikiana na serikali ili kuupokea utalii, huku akiwasihi wananchi kuendelea kutunza asili yao na vyakula vyao vya asili kwa lengo la kuvutia watalii nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Usafirishaji wa watalii Zanzibar (ZATO) Hassan Ali Mzee, alisema serikali imetoa kipaombele kutangaza kisiwa cha Pemba katika suala la zima la utalii.
Aidha aliwataka wananchi wa Pemba kuendeleza ukarimu wao, umoja, umoja mshikamano na amani iliyopo nchini ili kuvutia wageni, wakati wa uwekezaji utakapoanza.
Naye Mkurugenzi Masoko kutoka kamisheni ya Utalii Zanzibar Mohamed Mansour Nassora, alisema lengo la serikali ni kuongezaidadi ya watalii katika kisiwa cha Pemba.
Alisema hilo litaweza kufikiwa kutokana na mikakati mbali mbali ambayo kamisheni ya Utalii imejipanga, ikiwemo kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo Zanzibar.