Monday, November 25

ZBS yawashauri wajasiriamali Pemba kutengeneza bidhaa bora na zenye vigezo ili kupata alama ya ubora. .

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WAJASIRIAMALI kisiwani Pemba wametakiwa kutengeneza bidhaa bora zaidi ambazo zitakidhi vigezo vinavyohitajika katika kupata alama ya ubora ambayo itawasaidia kuuza bidhaa zao ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mkurugezi Dhamana Taasisi ya Viwango (ZBS) Pemba Salum Said Salum alisema, ipo haja kwa wajasiriamali kushindana katika kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu, hali ambayo itamsaidia kupata alama ya ubora kwa haraka.

Alisema kuwa, wafanyabiashara waliowengi Zanzibar hawajiamini kwa kile wanachokifanya, hivyo huzalisha bidhaa zilizo chini ya kiwango huku wakidai kwamba wananyimwa alama ya ubora.

“Tunao wajasiriamali wengi lakini wazalisha bidhaa chini ya kiwango na mazingira ya biashara sio sahihi, hivyo wanatakiwa wawe na ushindani wa kuzalisha bidhaa zenye ubora, hii itamsaidia kupata alama ya ubora kwa urahisi zaidi”, alisema MKurugenzi huyo.

Alieleza kuwa, ili mjasiriamali apate alama ya ubora, ZBS inaangalia mazingira yanayotumika kutengenezea bidhaa na ubora wa bidhaa yenyewe kwa kutumia mashine maalumu, ingawa wajasiriamali wanataka wapewe alama ya ubora hata ikiwa hakutimiza vigezo na masharti.

“Wanalalamika sana kwamba wanazalisha bidhaa zenye kiwango lakini hawapewi alama ya ubora, hawaangalii kwamba sisi tunatumia mashine kupima na sio kwa macho, ingawa imekuwa ni vigumu kuelewa”, alisema Mkurugenzi huyo.

Alieleza kuwa, wamekuwa wakijitahidi kutoa elimu kwa wajasiriamali hao kupitia wakaguzi wao wakati wanapokwenda kukagua bidhaa, hutumia nafasi hiyo kuwaelimisha.

“Tunazunguka Pemba nzima kuwatembelea wajasiriamali wetu na kuangalia hali zao na vile wanavyofanya na kuwaelekeza jinsi ya kufanya ili kuweza kufikia alama ya ubora”, alisema.

Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa, taasisi hiyo inafanya jitihada mbali mbali ya kuweza kuwasaidia wajasiriamali hao ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia tozo ya alama ya ubora, ambayo walikuwa wanalipa zaidi ya shilingi 900,000 ingawa kwa sasa imeshuka mpaka shilingi 150,000.

Alieleza kuwa, hiyo ni juhudi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutaka kuwapunguzia gharama za tozo wajasiriamali wake, ili waweze kufaidika na bidhaa wanazozalisha ambazo zinawasaidia kuwakwamu kiuchumi.

“Tunapokupa alama ya ubora tunaendelea kukutembelea na kukagua bidhaa ili tujue je unaendelea kama mwanzo na tukigundua bidhaa yako imepungua ubora tunakupokonya leseni ingawa mpaka sasa hivi hakuna aliepokonywa”, alifahamisha.

Aidha alisema, kwa sasa kuna wajasiriamali wameomba alama ya ubora, ambapo watatu wamefanikiwa kupata, wengine wamefeli na wengine majibu yao hayajarudi.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili ni wajasiriamali kutaka alama ya ubora licha ya kufikia viwango vinavyohitajika, kwani bado mazingira wanayofanyia hayako vizuri.

Changamoto nyengine zinazowakabili ni uhaba wa usafiri na wakaguzi, jambo ambalo linasababisha kutokufanyakazi kwa ufanisi zaidi na kutofikia lengo walilolikusudia.

“Tunayo gari moja na wakaguzi sita, hivyo tunahitaji angalau gari nyengine moja na wakaguzi kumi (10) na pikipiki, ili tutekeleze mipango ambayo tumejipangia”, alieleza Mkurugenzi huyo.

Ili wajasiriamali wapate alama ya ubora ipo haja ya kutimiza vigezo vinavyohitajika, jambo ambalo litawasaidia kusafirisha bidhaa zao nje ya nchi.