Friday, March 14

ZAWA watakiwa kulifanyia marekebisho ya haraka Bomba kuu la kusafirisha maji salama

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akielezea kusikitishwa kwake na jinsi ya Maji safi na salama yanavyopotea kwenye Bomba la kusafirisha Maji kupelekwa Saateni.

Uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { Zawa } kwa Kushirikianan na Wizara ya Maji na Nishati umetakiwa kulifanyia marekebisho ya haraka Bomba Kuu la kusafiria Maji Safi na salama liliopo pembezoni mwa Chem Chem ya Mto Pepo linalovuja kwa takriban Wiki Tatu sasa ili kunusuru Rasilmali hiyo muhimu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alitoa agizo hilo alipofanya ziara ya ghafla katika eneo hilo baada ya kupata Taarifa kutoka kwa Wananchi wema kuhusiana na umwagikaji ovyo wa Maji uliochukuwa masiku kadhaa.

Akitoa agizo la Wiki moja ya kuchukuliwa hatua za kuihami hali hiyo Mheshimiwa Hemed alisema wapo baadhi ya Wananchi katika maeneo tofauti Nchini bado wanaendelea kukosa huduma hiyo wakati baadhi ya sehemu inaendelea kumwagika ovyo bila ya kuchukuliwa hatua za dharura.

Alisema Maji yanayopotea katika eneo hilo lazima Viongozi hao wanaohusika na usimamizi wa Huduma hiyo waandae utaratibu utakaohakikisha unalitafutia suluhu tatizo hilo ambazo Serikali Kuu haipendelei kuliona linaendelea kuwepo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  alimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA}kumpangia kazi nyengine Mhandisi Mtendaji wa Mamlaka hiyo aliyopewa jukumu la kufanya ukaguzi wa kuipitia miundombunu ya Maji na akashindwa kutoia ripoti ya uwepo wa tatizo hilo.

Akitoa Taarifa ya Bomba hilo  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} Nd. Mussa Ramadhan Haji alisema Bomba hilo lililojengwa Mnamo Mwaka 1923  likiwa limeshadumu kwa takriban Miaka 97 sasa linahudumia Maji yanayotoka katika Chem chema ya Mtopepo na kupeleka katika Tangi Kuu liliopo Saateni.

Nd. Mussa alisema Bomba hilo lililokuwa chini ya Ardhi wakati wa ujenzi wake limezunguukwa na mmong’onyoko wa Ardhi pamoja na Ujenzi holela wa Nyumba za Makaazi hali iliyochangia chakaa na tayari limeshaanguka Zaidi ya mara mbili na kufanyiwa matengenezo makubwa.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA}alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba suluhu pekee ya kukabiliana na tatizo hilo ni kuingizwa katika Mradi Mkubwa wa kubadilishwa kwa Bomba hilo kazi ambayo endapo itafanyika Wananchi watalazimika kukosa huduma za Maji safi na salama si chini ya Wiki Tatu.

Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Banko Bwana Juma Bakari alisema tatizo hilo la uvujaji wa huduma hiyo ya maji safi wamelitolea taarifa kwenye Mamlaka husika n- ya Zawa kwa karibu Wiki Tatu sasa.

Hata hivyo Bwana Juma alionyesha masikitiko yake kutokana na Wahandisi wa Mamlaka ya Maji kuchukuwa muda mrefu kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo la uvujaji wa Maji.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alikagua eneo la Makaazi ya Wananchi liliopo Chumbuni Shehia ya Maruhubi ambalo Zaidi ya Nyumba 32 zimeathirika kutokana na kutuama kwa maji ya Mvua.

Akizungumza na Wananchi hao kutekeleza ahadi aliyoitoa ndani ya saa 48 kulitembelea eneo hilo Mheshimwa Hemed alisema Serikali Kuu itapeleka Wataalamu ndani ya Wiki Moja kwa ajili ya kulifanyia Utafiti eneo hilo kwa Awamu ya kwanza utakaosaidia njia ya kufanya katika kukabiliana na tatizo hilo.

Mheshimiwa Hemed alisema kama italazimika kuvunjwa kwa baadhi ya Nyumba kutokana na ushauri wa Kitaalamu Serikali itafikia hatua ya kufanya hivyo ili kunusuru athari kubwa inayoweza kuleta janga hapo baadae.

Alisema kutokana na hali halisi ya mazingira yalivyo lazima upatikane ushauri wa Kitaalamu utakaotoa muangaza kwa Serikali namna ya kuchukuwa hatua ili kunusuru kadhia hiyo inayoleta usumbufu na kudumu kwa  Zaidi ya Miaka 30 sasa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka Wananchi wenye Nyumba zinazolizunguuka eneo hilo kuwa na  Amani wakati Serikali itapolazimika kutekeleza wajibu wake kwa maslahi ya walio wengi.

Mmoja wa Wakaazi  wa asili wa eneo hilo Mzee Juma Haji alisema yeye tayari ameshaishi sehemu hiyo kwa Zaidi ya Miaka 30 na hakukuwa na tatizo la kutuiama kwa Maji ya Mvua kwa vile ulikuwepo Mtaro uliokuwa ukisafirisha Maji kutoka eneo hilo na kuyapeleka Maruhubi na Saateni.

Mzee Haji alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa mazingira halisi ya sasa Mtaro huo umeshindwa kufanya Kazi na matokeo yake maji ya Mvua yanayotokea katioka maeneo ya Chumbuni, Cotex na Karakana yanaishi hapo kwa muda mrefu sasa.

Othman Khamis Ame.

Ofisi ya Makamu wa Pili wa wa Zanzibar.