Monday, November 25

Acheni kulimbikiza madeni kwa wasambazaji wa dawa – Mhe Hemed

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdalla akimsikiliza Mkurugenzi wa bohari kuu ya dawa Zanzibar Bohari kuu ya dawa Dr Zahran Ali Hamad akimueleza namna ya uingizwaji na utokaji wa dawa katika Ofisi zao zilizopo Maruhubi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akitoa maelekezo kwa watendaji wa bohari kuu ya dawa juu ya kuangamiza dawa na vifaa tiba vilivyopitwa na wakati alipofanya ziara  katika Bohari hiyo maruhubi.

Mhe. Hemed akimsikiliza Mkurugenzi wa Yassin And Sons co. Limited Ndugu Othman Abdallah akimpa maelezo juu ya maendeleo ya ujenzi wa jengo la mnadani Darajani alipofika kukagua na kujua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akisalimiana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Riziki Pembe Juma alipofika kukagua ujenzi wa nyumba ya Mnadani Darajani.

Na Abdulrahman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameutaka uongozi wa wizara ya afya  kuacha tabia ya Kulimbikiza madeni kwa wasambazaji wa dawa ili kuondosha usumbufu wa upatikanaji wa dawa  hali inayopelekea malalamiko  kutoka kwa wananchi .

Mhe. Hemed ameeleza hayo wakati alipofanya ziara ya kuangalia hali ya uingizwaji na usambazwaji  wa Dawa Katika Bohari Kuu  ili yopo  Maruhubi Jijini Zanzibar.

Amesema hajafurahishwa na hali ya ufanyaji kazi kwa baadhi ya viongozi katika wizara hiyo  kwa kutowalipa wasambazaji wa Dawa fedha kwa wakati hali ambayo serikali  tayari imeshatenga fedha hizo  kwa ajili ya malipo ya dawa hizo hali  inayopelekea kudorora kwa huduma za afya nchini.

Amesema umefika wakati kila mmoja kwa nafasi yake kuangalia namna bora ya kutumia fedha hizo, kwa kufuata utaratibu mzuri wa kuhakikisha wasambazaji wanalipwa fedha zao kwa wakati  na kueleza kuwa Serikali iko tayari kuongeza fedha hizo  kwa ajili ya ununuzi wa  dawa zinapohitajika ili kuboresha huduma ya afya kwa  wananchi.

Amesema hali hiyo  inasababishwa na mfumo mbaya wa uendeshaji wa Wizara hiyo, jambo ambalo linasababisha wananchi kupunguza Imani kwa wizara hiyo. Aidha,  Mheshimiwa Hemed amewataka kuachana na kufanya kazi kwa mazoea ili kurahisisha huduma hizo kwa wananchi bila ya usumbufu wowote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema serikali imegundua uwepo wa  ulipaji wa madeni kiholela bila ya kufuata taratibu zilizopo ambapo inapelekea wasambazaji kulipwa zaidi ya mara moja, hali inayopelekea upotevu wa fedha za serikali.

Kuhusu upatikanaji wa Dawa vituoni  Mhe. Hemed ameuagiza uongozi huo kuhakikisha Dawa zote zinapatikana kwa wakati, na kukemea tabia ya wananchi kununulishwa Dawa hali ya kuwa serikali inamudu ununuzi wa Dawa hizo, na kuwataka kuagiza vifaa tiba ambavyo vimekamilika.

Mhe. Hemed amewataka wataalamu kupitia maombi ya Dawa yanayotoka Vituoni kuyapitia upya maombi hayo, ili kupunguza mrundikano wa dawa katika bohari kuu wakati katika vituo vya afya dawa hizo hazipatikani.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali imejitahidi kuweka wataalamu katika maeneo mbali mbali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila ya usumbufu, na kuwataka wataalamu hao kufanya kazi  kwa kutumia taaluma zao ili kufikia lengo la serikali ya Awamu ya Nane la kuwatumikia wananchi wake.

Kuhusu Dawa zilizomaliza muda wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameuagiza uongozi wa wizara ya afya kupitia taasisi ya bohari kuu ya Dawa  kushirikiana na  wakala wa  chakula, dawa na Vipodozi ili  kuziangamiza Dawa ambazo zimeisha muda wa matumizi kwa lengo la kuimarisha usalama wa Afya ya watumishi wa Bohari hiyo na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkurugenzi kinga na Tiba Wizara ya Afya Amour Mohammed Suleiman  Amemueleza Makamu wa Pili kuwa hali ya upatikanaji wa Huduma ya Dawa vituoni hairidhishi hususan Dawa zinazotumika mara kwa mara na kuomba kuwa na utaratibu mzuri wa kuagiza Dawa hizo.

Nae Mkurugenzi  wa Bohari kuu ya madawa Zanzibar Dr Zahran Ali Hamad ameeleza kuwa Dawa lzinazoingia Bohari hupokelewa na kuingizwa katika Mfumo jambo  ambalo husaidia kufahamu Dawa zilizopo na zinazoingia kulingana na  mahitaji kwa ujumla.

Wakati Huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametembelea na kukagua Ujenzi wa jengo la Mnadani Darajani Jijini Zanzibar.

Katika ziara hiyo Mhe. Hemed amsema lengo la ukarabati wa  jengo hilo ni kuufanya mji uwe na muonekano mzuri na kumtaka mkandarasi wa ujenzi huo Yassin and Sons kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwangoilivyowekwa ili kuweza kuleta manufaa kwa wananchi.