NA ABDI SULEIMAN.
KAMATI ya Uchumi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, imepongeza juhudi zilizochukuliwa na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kuanzisha mfumo wa utoaji wa risiti za kieletronik kwa wafanyabiashara, ili kuhakikisha mapato ya serikali yanapatikana.
Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Sabiha Filfil Thani, wakati alipokua akitoa majumuisho ya kamati hiyo huko katika ofisi za ZRB Gombani Wilaya ya Chake Chake.
Mwenyekiti huyo alisema mfumo huo ulioanzishwa ni mzuri na utasaidia kupatikana kwa mapato ya serikali kutoka kwa wafanyabiashara, jambo ambalo hapo nyumba serikali ilikuwa ikiyakosa.
Aidha aliitaka ZRB kuhakikisha inaongeza bidii katika ukusanyaji wa mapato ya serikali, ili kuendana na malengo ya bajeti walioyomba katika baraza la wawakilishi.
“Mimi binafsi nawashukuru ZRB kwa kuja na mfu muu wa utoaji wa risiti za kieletronik, jambo jema mumeanza na mahoteli na wafanyabiashara wakubwa, huku ndiko pesa ya serikali inakopotea “alisema.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Juma Makungu Juma, alisema uwepo wamashine za VFMS,utasaidia upatikanaji wa fedha za serikali ambazo zimekua zikikosekana kutoka kwa wafanyabiashara.
Nao baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo Nadir Abdullatif Yussuf na Hussein Ibrahim Makungu, walipongeza mfumo huo ambao utakuwa mkali katika utoaji wa risiti pale miamala ya manunuzi inapofanyika baina ya mfanya biashara na mteja wake.
Katika hatua nyengine Mjumbe wa Kamati hiyo Nadir Abdullatif Yussuf, alisema ifike wakati watu walazimishwe katika uchukuaji wa mashine hizo kwa ajili ya kulipia kodi na sio kutoavisingizio ambavyo havifai.
Alisema katika ziara inayofuata vizuri kutembea na askari kama zilivyokamati za wabunge, kwa wale wawekezaji ambao ni wakaidi na wagumu kufuata maagizo ya serikali na anapoteza kodi za fedha vizuri kuchukuliwa na polisi ili kujibu hoja.
“Haiwezekani meneja wa Hoteli ya Aiyana akawa anadanganya kama vile, lazima meneja yule kushuhulikiwa inaonekana ni mgumu kulipa fedha za serikali kama alivyobabaisha katika utumiaji wa mashine, zanzibar ni zanzibar tusiifananishe na Dubai,”alisema.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Jamal Kassim Ali, alisema bado ZRB wanakazi kubwa ya kufanya katika kuhakikisha wanakusanya ipasavyo mapato ya serikali.
Alisema elimu inapaswa itolewa ipasavyo pamoja na usajili wa walipakodi, inapaswa kuendelezwa kwa mujibu wa sheria ili kufikia malengo yao.
Waziri Jamali alisema ZRB wanapaswa kujipanga kuhakikisha kila anayestahiki kupatiwa mashine hizo za VFMS anapatiwa, huku wakiendelea kuboresha mfumo huo ili kujuwa mgeni anatoka wapi, anakaa siku ngapi na hoteli gani anafikia.
“Kwanza tumelazimika kuanza na wafanyabiasha ambao waliosajiliwa katika mfumo wa VIT, lengo ni kukusanya kodi za serikali zote zinazostahiki kukusanywa,”alisema.
Hata hivyo aliitaka bodi hiyo kutoa wataalamu kwenda kujifunza nje ya nchi juu ya mifumo hiyo inavyo kwenda, kwa upande wa uwekezaji alisema serikali tayari imeshakodisha kisiwa cha njau, ambapo mwekezaji huyo atahakikisha anajenga vyumba vingi vya chini ya bahari na hoteli ya kisasa.
Naye kamishana wa ZRB Salum Yussuf Ali, alisema mfumo huo uwezakuondosha suala la udanganyifu kwenye ukusanyaji wa kodi, kwani mfanyabiasha kila anachokifanya kinaonekana kwenye mtandao moja kwa moja.
Aidha aliwashukuru wajumbe hao kwa kuukubali mfumo huo wa utoaji wa risiti, huku akiwataka wajumbe hao kuwashajihisha wafanyabiashara kuhakikisha wanatoa risiti za kieletroniki baada ya kufanya miamala na mteja wake.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa IT kutoka ZRB Harith Abdiazizi Ahmada, alisema watahakikisha wanatumia Video za mitandao katika kutoa elimu kwa jamii juu ya suala zima la mwananchi kudai risiti baada ya kulipa.
Alisema serikali inatoa mfumo bure kwa lengo la kupata kodi, pamoja na kufanya maboresho makubwa, ikizingatiw abaadhi ya nchi zinatoa mifumo kwa kulipia.
Nae meneja wa Hoteli ya The Manter Resort Zamda Hssein, amepongeza juhudi zilizochukuliwa na serikali za kuhakikisha wanaanzisha mfumo wa utoaji wa risiti za kieletronik, kwa lengo la kupata mapato yake kutoka kwa wafanya biashara.