Sunday, November 24

Tanzania yaanika sababu ya kuwa na Simba wengi duniani

Rais wa Jumuiya ya Uwindaji ya Kimataifa, (SCI), Sven Lindqueast ameitaja Tanzania kuwa ni nchi yenye  nusu ya simba wote Duniani katika Mkutano wa 50 wa Mwaka wa Uwindaji wa Kitalii unaoendelea kufanyika jijini Las Vegas, Marekani

Rais huyo Bw. Sven Lindquest amesema kwa hatua hiyo anaipongeza Tanzania kwa juhudi kubwa za uhifadhi uliopelekea wingi wa wanyamapori hao.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amesisitiza kuwa nusu ya simba wote wapo Tanzania  kutokana na uimara wa Serikali katika shughuli za  uhifadhi

Amesema kuimarika kwa shughuli za uhifadhi hususani kwa Wanyamapori walao nyasi ni moja ya sababu ya Tanzania kuwa na Simba wengi  hivyo imepelekea  Simba nao  kuongezeka kutokana na uhakika wa  chakula cha kutosha

Amefafanua kuwa Simba hula wanyamapori walao nyasi na wanyamapori hao wamekuwa wengi kutokana na uwepo wa nyasi za kutosha na usimamizi bora wa maeneo ya Hifadhi

” Kubadilishwa  mfumo kutoka wa kirai kwenda katika mfumo wa kijeshi kwa Watumishi wote wanaosimamia maeneo ya Hifadhi ni moja ya sababu ya simba kuongezeka kwa Simba nchini Tanzania” alisema Dkt.Ndumbaro

Waziri  Ndumbaro  amesisitiza kuwa Tanzania imefanikiwa kuwa simba wengi kutokana na Serikali kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini kwa kuitengea Wizara ya Maliasili na Utalii bajeti ya kutosha inayotumika katika kuendesha operesheni mbalimbali za kukabiliana na ujangili

Amesema Serikali imeweza kufanikiwa kukomesha tatizo la  ujangili kwa  zaidi ya asilimia 90 huku akisisitiza kuwa inatarajia kumaliza kabisa tatizo la  ujangili kufikia asilimia 100% ifikapo mwaka 2025.

” Uthubutu wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan wa kuwa bega kwa bega na Wizara imekuwa chachu kwa Tanzania kuzidi kuongoza kwa kuwa na simba wengi Duniani”