NA ZUHURA JUMA, PEMBA
KAMATI ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imelitaka Shirika la Nyumba kisiwani Pemba, kuzifanyia matengenezo nyumba chakavu sambamba na kujenga nyumba mpya, ili kujiendesha kibiashara.
Wakitoa mapendekezo mara baada ya kuwasilishwa ripoti ya shirika hilo mbele ya Mwenyekiti wa kamati hiyo Ali Suleiman Ameir, wanakamati hao walisema ipo haja kwa Shirika hilo kubadilisha mfumo ili liweze kujipatia mapato yake.
Walisema kuwa, wakati umefika sasa kwa Shirika hilo kuchukua mkopo kwa ajili ya kuzitengeneza nyumba zilizo chakavu pamoja na kujenga nyengine mpya ili kujiendesha kibiashara zaidi, jambo ambalo litasaidia kupata mapato kwa urahisi.
Walieleza kuwa, iwapo nyumba hizo zitakuwa nzuri, wateja wake hawatokuwa na sababu ya kutokulipa na hivyo itasaidia kupunguza malimbikizo ya madeni kwa wadaiwa sugu.
Mwakilishi wa Jimbo la Pandani Profesa Omar Fakih Hamad alisema kuwa, uchakavu wa nyumba isiwe sababu ya nyumba hizo kuendelea kuharibiwa, hivyo ipo haja ya kuchukua mkopo waweze kuzifanyia matengenezo nyumba hizo, ili ziwe nzuri.
“Shirika lipo, kwa hiyo hakuna sababu ya nyumba hizo kuwa chakavu, tufanye juhudi mbali mbali kuhakikisha nyumba zinakuwa nzuri, pia tuanzishe mradi wa kujenga nyumba mpya, hii itasaidia Shirika kujiendesha kibiashara”, alieleza Profesa huyo.
Kwa upande wake mwakilishi wa jimbo la Chwaka Issa Haji Ussi (Gavu) alilitaka Shirika hilo kusimamia ulipaji wa kodi, ili liweze kujiendesha kwani kuna malimbikizo makubwa ya madeni.
“Shirika lina nyumba nyingi lakini hatuwezi kusimamia, hivyo tunatakiwa tujitathmini upya juu ya kufanya mageuzi, uwezekano wa kulipa kodi kwa wateja wenu ni mdogo sana, hivyo zifanyieni matengenezo nyumba hizo”, alisema mwakilishi huyo.
Nae mwakilishi wa jimbo la Wete Harus Said Suleiman alieleza kuwa, pamoja na jitihada zinazofanywa na shirika hilo lakini bado nyumba haziridhishi, kwani ni chakavu sana.
“Shirika liwe na utaratibu wa kuzikagua nyumba ambazo zimefanyiwa matengenezo, kwani wateja wao wanazitumia kinyume na inavyotakiwa”, alishauri mwakilishi huyo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ali Suteiman Ameir aliliagiza Shirika hilo kukaa na kutafakari ili kuondosha changamoto zinazowakabili na kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi.
“Kwa nini wateja mumewaacha wasilipe muda wote mpaka wanakuwa na madeni makubwa, mujipange upya kuhakikisha wateja wote wanalipa madeni, sambamba na nyumba hizo kuzifanyia matengenezo”, alisema Mwenyekiti huyo.
Akizungumza katika kikao hicho Afisa Mdhamini Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Pemba Bakar Ali Bakar alifahamisha, wamekuwa wakiwafahamisha wateja wenye malimbikizo ya madeni namna ya kulipa, ingawa wamekuwa wakipuuza, jambo ambalo linawarudisha nyuma katika shughuli zao, kwani fedha zinazopatikana ndizo ambazo wanafanyia matengenezo.
Mapema akiwasilisha ripoti hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba Pemba Ali Mgau Kombo alisema, hadi kufikia Disemba 2021 Shirika linawadai wateja wake shilingi 786,994,400.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili ni ukosefu wa gari ya kufuatilia, ukosefu wa wataalamu wa ujenzi, wakadiriaji majengo, malimbikizo makubwa ya madeni na ulipaji kodi usioridhisha pamoja na uchakavu wa nyumba nyingi za Shirika ambao unapelekea mazingira hatarishi kwa wapangaji.
Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba mwaka 2021 Shirika lilikadiria kukusanya shilingi 99,750,000 kutoka katika vianzio vyake vya mapato na hadi kufikia Disemba lilikusanya shilingi 62,719,000 sawa na asilimia 62.86 ya makadirio ya makusanyo.