Monday, November 25

Rais Dk Hussein Mwinyi awaapisha viongozi aliowateuwa karibuni Ikulu-Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaapisha watendaji mbali mbali aliowateua hivi karibuni kushika nyadhifa zao.

 

Hafla hiyo ya kiapo imefanyika Ikulu Jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na Viongozi wakuu wa Kitaifa, Mawaziri, Viongozi wa Vyama vya siasa, Viongozi wa Dini pamoja na Wanafamilia.

 

Viongozi walioapishwa kushika nyadhifa hizo ni pamoja na Jaji Aziza Idd Sued alieteliwa kuwa Mwenyekiti wa Mahakama ya Rufaa ya Idara Maalum za SMZ pamoja na Dk. Said Seif Mzee alieteuliwa kuwa Mhasibu Mkuu wa Serikali Zanzibar katika Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango.

 

Mwengine ni Rahma Salim Mahafoudh alieteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar katika Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango.

 

Miongoni mwa Viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na  Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi  Zena Ahmeid Said, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Mawaziri, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Vyama vya siasa pamoja na Wanafamilia.

 

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,   Dk. Hussein Ali Mwinyi amefanya mahojiano na waandishi  kutoka vyombo mbali mbali vya habari hapa nchini.

 

Katika hafla hiyo iliofanyika Ikulu Jijini Zanzibar, Dk. Mwinyi alijibu maswali mbali mbali pamoja na kupokea ushauri kutoka kwa waandishi wa habari  katika nyanja za siasa, uwekezaji, ustawi wa jamii, michezo, ulinzi na usalama pamoja na kutoa rambi rambi kwa waandishi wa habari watano  waliofariki dunia Mkoani Singida hivi karibuni, wakati walipokuwa katika safari ya kikazi kuelekea Chato Mkoa wa Geita.

 

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar