Sunday, November 24

PECEO yawapa mafunzo wanawake walio katika vikundi vya uzalishaji na vikoba juu ya umiliki wa ardhi.

 

NA ABDI SULEIMAN.

WANAWAKE Kisiwani Pemba, wamesema kuwa ukosefu wa elimu juu ya umiliki wa ardhi na ucheleweshwaji wa Mirathi, ni moja ya sababu inayopelekea migogoro ya ardhi kuongezeka katika jamii.

Aidha wamesema kuwa yote hutokea baada ya mmoja ya wanafamilia kufariki dunia, na mali iliyoachwa kusimamiwa na wakubwa wa familia huku wadogo wakiendelea kukosa haki hizo.

Wakizungumza katika mkutano wa siku mbili huko Gombani mjini Chake Chake, juu ya kutoa elimu ya umiliki wa ardhi, kwa akina mama waliomo katika vikundi vya uzalishaji na vikoba, ili kuweza kutambua haki zao za msingi za kutetea kumiliki ardhi na waweze kujikomboa na umaskini, mkutano huo ulioandaliwa meandaliwa na jumuiya ya PECEO kwa ufadhili wa FCS.

Asha Abdalla Said Kutoka shehia ya Ngachani alisema changamoto nyengine inayopelekea wanawake kutokumiliki mali ni Imani za Kishirika, wanakuwa na hofu kwenda kudai huku wakihofia kupewa shetani na kuanza kumtesa sababu ni mali.

Alisema jengine ni mwanamke kuonekana ni mtu duni juu ya umiliki wa ardhi, kwa kuwa hawezi kuisimamia na kulinda mali hiyo jambo ambalo hupelekea kukosa haki yake.

Naye Zuwena Mohamed Ali kutoka Shehia ya Chambani, wanawake wenyewe kutokujiamini na kuwa kitu kimoja katika kudai haki hiyo ya umiliki wa ardhi.

Kwa upande wake afisa Usajili ardhi na utoaji wa hati miliki kutoka Kamisheni ya Ardhi Pemba Yussuf Hamad Kombo, alisema kamisheni ya ardhi ndio taasisi pekee yenye mamlaka ya kumilikisha ardhi nchini.

Alisema uhalali wa ardhi ya pale mtu anatakapopata hati ya umiliki wa ardhi, kwani bila ya kuwepo kwa ardhi hakuna maendeleo yoyote yanaweza kufikiwa.

Mratibu wa Mradi wa ushawishi wa upatikanaji wa haki za umiliki wa ardhi kwa wanawake Pemba, Juma Said Ali alisema bado wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa wakati wanapotaka kumiliki ardhi kutoka katika familia.

Alisema baada ya mmoja ya wanafamilia kufariki, kaka wa familia huhodhi mali zote na kushindwa kuwapatia ndugu zao ikiwemo wanawake.

“Leo utaona mtu anachuma karafuu na kuuza hupata zaidi ya milioni, ikizingatiwa mali haijarithiwa hapo mwanamke hukosa au hupata kidogo kulingana na mali hiyo,”alisema.

Aidha alisema jumuiya ya PECEO ipo msatari wa mbele katika kusaidia serikali, mambo mbali mbali ikiwemo suala zima la elimu na kufikia maendeleo yaliyokusudiwa.

Mafunzo hayo yametolewa na Jumuiya ya kuwawezesha Jamii Pemba (PECEO), kwa Ufadhili wa The Foundation for civil society na kufanyika mjini Chake Chake.

MWISHO