(PICHA NA HAJI NASSOR)
NA HAJI NASSOR, PEMBA
MKUU wa Mkoa wa kusini Pemba, Mattar Zahor Massoud, amewataka majaji, mahakim na wanasheria wengine, ambao hawajaamua kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa, kutafuta kazi nyingine ya kufanya, kwani wakiendelea, hivyo ni kuipotezea uaminifu serikali kwa wananchi.
Alisema, wapo baadhi yao wamekuwa hawawezi kufanyakazi pasi na kujihusisha na rushwa, na kusababisha kuwapotezea haki wengine jambo ambalo wananchi hupoteza imani na muhimili huo.
Mkuu huyo wa Mkoa aliyasema hayo jana ukumbi wa kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake, kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria Zanzibar ambapo kwa Pemba kilifanyika hapo.
Alisema, inashangaaza kuona kuna jaji au hakimu, akijua kuwa upande usio na haki ndio anakotoa uamuzi wa kesi, kubwa kwa kufuata maslahi yake.
“Inashangaaza kuona kuna Jaji au hakimu anajihusisha na kupinda sheria, kwa kuchukua rushwa, na kuacha kutoa haki kwa upande unaostahiki, hili linaitia doa mahakama na serikali kuu,’’alieleza.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa aliitaka Idara ya mahakama kuangali mifumo yao ya sheria, uendeshaji wa kesi ikiwa hauwakwazi wananchi.
Alieleza kuwa, inawezekana kuna mdororo mkubwa wa uendeshaji wa kesi na hasa eneo la mashahidi, sasa lazima Mahakama iangalie sababu za wananchi kutofika mahakamani.
Aidha aliwataka wananchi, kuendelea kushirikiana kwa karibu na mahakama ili kufika mahakamani kutoa ushahidi hasa kwa kesi za dawa za kulevya, udhalilishaji na wizi.
Mapema Jaji mkaazi wa mahakama kuu Pemba Ibrahim Mzee Ibrahim, alisema kabla ya kufikia kilele hicho waliwatembelea wananchi na kuwapa elimu.
Alisema walifika kijiji cha Pujini kuzungumza na wananchi juu ya athari za dawa za kulevya, udhalilishaji na kuwashajihisha kufika mahakamani kutoa ushahidi.
Kwa upande wa Mwanasheria dhamana wa Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Pemba Ali Haidar Mohamed, alisema wakati umefika sasa kwa mahakama kuongeza kasi ya usikilizaji kesi.
Alisema, zipo kesi kadhaa zimeshachukua muda mrefu, ikiwemo ya mtuhumiwa anaedaiwa kumuua mama yake tokea mwaka 2008 na hadi alipofariki mwaka 2020 kesi yake haikusikilizwa.
“Sisi ofisi ya DPP tumepata imani kubwa ya kesi hasa za mahakama kuu kuendeshwa kwa haraka, baada ya serikali kumuweka jaji kisiwani hapa,’’alieleza.
Hata hivyo alisema ofisi hiyo inasikitishwa na tabia ya baadhi ya wananchi kufutisha kesi jambo ambalo linapoteza haki kwa watendewa wa makosa na hasa watoto.
Afisa Mdhamini wizara ya nchi afisi ya rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Pemba Halima Ali Khamis liwataka wananchi kuendelea kuitunza amani iliyopo, ili shughuli za kitaifa zilizopangwa zifanikiwe.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo, akiwemo Hawa Iddi Mshamba na Hassina Omar Shehe walisema, ni vyema katika kilele kama hicho kuwasilishwe kwa baadhi ya sheria.
“Kama kuna sheria ambayo inatukwaza sisi wakati tunapokusanya ushahidi au kutoa ushahidi, Mahakam ingekuwa inawasilishwa na kutoa maoni yetu.
Awali kulifuatiwa na matembezi ya wanasheria, mahakimu, mawakili wa serikali na kujitegemea na wanasheria wa mawizara na kisha Jaji mkaazi kukagua gwaride maalum.