NA ZUHURA JUMA, PEMBA
KAMATI ya soko la samaki na mboga mboga Tumbe Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, imesema imedhamiria kujenga skuli ya maandalizi na msingi, ili kuwapunguzia watoto masafa marefu ya kuifuata huduma hiyo.
Kamati hiyo imesema kuwa, walikaa pamoja na kutafakari kitu cha kufanya katika kuisaidia Serikali kufikisha huduma za kijamii kwa wananchi, ambapo walipendekeza kujenga skuli.
Walisema kuwa, watoto wa shehia mbili za Tumbe huifuata huduma hiyo masafa marefu, hivyo wameona ni vyema angalau kuwapunguzia masafa hayo wanafunzi wa maandalizi na msingi kutokana na kuwa wao ni wadogo.
Walieleza kuwa, wamekuwa wakikusanya fedha kutoka kwa wavuvi wanaotumia bandari ya Tumbe na kuziingiza katika akaunti yao ya soko, hivyo wameona kiasi cha fedha walichonacho ni vyema wakaisaidia Serikali katika kuwafikishia wananchi huduma za kijamii.
Katibu wa Kamati ya Soko hilo Rashid Khatib Hamad alisema, kwa sasa kwenye akaunti yao kuna zaidi ya shilingi milioni 19 ambazo wamezikusanya tangu mwaka 2016.
“Kamati hii ilianzishwa na wavuvi wenyewe na wameiridhia, hivyo fedha tunazokusanya hapa kila siku, inapofika mwisho wa mwezi asilimia 20 inakwenda halmashauri ya Wilaya yetu na asilimia 80 inapelekwa kwenye akaunti ya soko na ndio hiyo ambayo tunataka tujenge skuli”, alisema mwenyekiti huyo.
Alieleza kuwa, wameshaona eneo la kujenga skuli hiyo ingawa mmiliki wa eneo hilo anahitaji apatiwe angalau eneo jengine litakalomsaidia kufanya shughuli zake za kumpatia kipato ikiwa ni pamoja na kilimo.
“Kwa kushirikiana na Jumuiya yetu ya Maendeleo ya Tumbe, tupo kwenye harakati za kumtafutia eneo jengine mwananchi huyo japo la Serikali, ili tupate kuanza ujenzi huo wa skuli”, alisema Katibu huyo.
Alisema, makusanyo yote yanayopatikani yanatokana na mnada, ambapo wanayaweka kwa ajili ya matumizi ya soko, kuisaidia jamii pamoja na kuipatia Serikali mapato yake, ambapo kila mvuvi anatakiwa kutoa asilimia tatu ya mauzo yake kwa siku.
Aidha alisema kuwa, hivi karibuni walikwenda kufungua akauti katika benki ya CRDB kwa ajili ya kuwawezesha na kuwaboresha wavuvi kwa kuwatafutia mashine na boti za kisasa ambazo zitawawezesha kufika mbali na kuvua samaki wakubwa.
Aliwataka wavuvi hao waelewe kwamba kinachofanyika baada ya makusanyo hayo ni suala la maendeleo kwa jamii, hivyo wawe wepesi katika kuchangia kwa ajili ya soko na jamii ya Tumbe kwa ujumla.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya wavuvi Tumbe Omar Hamad Salim alisema yeye anahusika na kukusanya fedha kwa kila boti ambazo zinatia nanga katika bandari ya Tumbe.
“Fedha hizi zinatusaidia pale ambapo wavuvi wamepatwa na dharura, hivyo tunaweka mafuta kwenye boti na kwenda kuwaokoa na pia tunachangia kwenye huduma za kijamii kwa kushirikiana na kamati yetu ya soko”, alisema Katibu huyo.
Alieleza, hivi karibuni kuna kiwanja kimeuzwa kwa ajili ya kujengwa hospitali ya Tumbe, hivyo walitakiwa wapeleke laki saba, ambapo tayari wameshazitoa sambamba na kusaidia mipira ya maji kwa ajili ya kufikisha huduma hiyo msikitini.
Kwa upande wao wavuvi Hamad Suleiman Mwinyi na Horera Suleiman Zahran wamesema ni jambo zuri ambalo wanataka kulifanya, kwani itakuwa wamechangia kuimarisha huduma za kijamii katika shehia zao.
Mwananchi Khadija Suleyum mkaazi wa Tumbe alisema kuwa, iwapo watajenga skuli hiyo watakuwa wameisaidia sana jamii, kwani watoto wadogo wanakwenda skuli masafa marefu.
Nae Ali Hassan Sheha alieleza kuwa kamati hiyo ikiwa itajenga skuli, wananchi wataelewa kwamba mapato yanayopatikana kwa wavuvi hayaliwi na mtu mmoja bali ni kwa manufaa ya wanajamii wote wa Tumbe.
MWISHO.