Tuesday, November 26

Akamatwa na misokoto 60 ya dawa za kulevya.

NA MWANDISHI WETU, PEMBA

JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba limemkamata kijana Hemed Omar Ali mwenye umri wa miaka 21 mkaazi wa Konde Chanjaani baada ya kupatikana na misokoto 60 ya dawa za kulevya aina ya bangi yakiwa nyumbani kwake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Juma Sadi Khamis alisema, mtuhumiwa huyo amekamatwa Febuari 6 mwaka huu majira ya saa 9:30 jioni huko nyumbani kwake Konde Chanjaani Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba alipatikana na misokoto 60 ya bangi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kamanda huyo alisema, mtuhumiwa huyo ni maarufu kwa uuzaji wa madawa ya kulevya, hivyo Jeshi la Polisi limemshikilia baada ya kufanya operesheni katika maendeleo mbali mbali ya Mkoa.

“Pamoja na Jeshi la Polisi kufanya msako katika maeneo yote ya Mkoa, lakini walikuwa hawajafanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo, kwa bahati nzuri tulimkamata na tunaendelea mahojiano”, alieleza Kamanda huyo.

Kamanda Sadi alieleza kuwa, upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na mara tu utakapokamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Aliwataka vijana wa Konde kuacha tabia ya kuuza madawa ya kulevya na kuwataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi, ili wapatikane wauzaji, jambo ambalo litasaidia kuondosha biashara hiyo haramu.

“Tusiwafiche wauzaji kwani tutawaumiza watoto wetu, hapa Konde kuna vijana wengi wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, hivyo ni vyema tushirikiane kukomesha”, alisema Kamanda huyo.

Tangu kuanza mwaka huu ni tukio la nne kwa vijana kukamatwa na madawa ya kulevya huko Konde Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.