MWENYEKITI wa Bodi ya Ligi Kuu Bara, Steven Mnguto, ameibuka na kusema licha ya wadhamini wenza Kampuni ya GSM kutangaza kujiondoa katika udhamini lakini hakuna klabu yoyote iliyolipwa.
Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tangu GSM watangaze kujiondoa kudhamini klabu za ligi ambazo awali waliingia mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh 2.1Bil.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mnguto alisema kuwa, hilo suala wamepanga kulizungumza hivi karibuni
mara baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) watakapokutana.Mnguto alisema kuwa, wanasubiria wanasheria wao walipitie suala hilo na mwisho wa siku watalitolea ufafanuzi kwa undani.
“Kiukweli tangu tuliposaini mkataba na GSM nikiri klabu hazijapata chochote. Klabu zimeitangaza GSM kwa muda wa miezi mitatu sasa, kwa hiyo tunasubiri wanasheria walipitie suala hilo tujue tunafanyaje.
“Hata suala la zile nembo kwenye mabega sijui kama zinaweza kutolewa haraka lakini hata hilo litafanyiwa
kazi kisheria,” alisema Mnguto.
Naye Mkurugenzi wa Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura, akizungumzia hilo alisema: “Sisi
baada ya kupata barua kutoka GSM, suala la mkataba ni Bodi ya Ligi na ni vema akatafutwa Mnguto lakini
kwa upande wa sisi TFF hatuwezi kuzungumzia kila jambo.
“Tayari tumetoa tamko letu jana (juzi) kuhusiana na hilo baada ya kupata barua GSM.”
Juzi TFF ilitoa taarifa kuwa, Februari 7, mwaka huu walipokea barua ya kuvunja mkataba wa udhamini mwenza wa Ligi Kuu Bara ya NBC kutoka Kampuni ya GSM, hivyo Shirikisho hilo linafanyia kazi barua hiyo na litatoa taarifa kwa wadau.