Monday, November 25

KMKM yaiomba SMZ kutafta namna ya kusaidia Boti zinazosafirisha wananchi katika Visiwa vidogo vidogo Pemba.

NA ABDI SULEIMAN.

KIKOSI cha KMKM Kisiwani Pemba kimeiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuangalia namna ya kuzisaidia Boti zinazosafirisha wananchi katika Visiwa vidogo vidogo, ndani ya Kisiwa cha Pemba katika kumudu gharama za uendeshaji.

Kikosi hicho kimesema tatizo kubwa la kusimamia boti hizo ni ukosefu wa fedha za uendeshaji, huku wakishindwa kujuwa vitaendelea kutoa huduma.

Hayo yameelezwa na Afisa Operesheni wa Kikosi cha KMKM Kisiwani Pemba Muharami Amani Mgeni, wakati akitoa maelezo kwa wajumbe wa kamati ya Kuchunguza na kudhibiti hesabu za Serikali ya Baraza la Wawakilishi huko Bandarini Mkoani.

Alisema vyombo hivyo walikabidhiwa KMKM kwa lengo la kuviendesha  na kuvitunza, lakini suala la uwezeshaji linakwenda kwa wakusanyaji wa mapato, kutokana na utaratibu ulivyo hayawezi kukidhi gharama hizo.

“Sisi tulikabidhiwa hivi vyombo kuviendesha na kuvitunza, suala la uwezeshaji ndio linalohitajika na sisi kwetu huo utaratibu haupo,”alisema.

Akizungumzia juu ya suala la ukusanyaji wa mapato, alisema kwa upande wa Mkoa wa Kusini kuna kamati maalum za ukusanyaji wa mapato kutoka shehiya husika, ndio dhamana wa kukamata mapato hayo jambo ambalo linakuwa gumu kufidia gharama za uendeshaji pale mapato hayo yanapokuwa hayatoshelezi.

“kwa upande wa Mkoa wa kaskazini boti, hizo ziko chini ya halmashauri lakini pia mapato hayake hayawezi kukidhi gharama hizo,” alisema.

Akizungumzia utaratibu wa uendeshaji wa Boti hizo, Mkuu wa Wilaya ya Wete Hamad Omar Bakar, alisema hivi sasa boti hizo zinafanya kazi kihasara, kwani mapato yake hayawezi kumudu gharama za uendeshaji.

“Kiukweli hizi boti ni nzuri na zinasaidia sana wananchi katika suala la kuwavusha, lakini changamoto kubwa iliyopo ni uwendeshaji wake ni hasara mpaka sasa,”alisema.

Naye Mkurugenzi Baraza la Mji Wete Salma Abuu Hamad, alisema kutokana na mapato madogo yanayoingia kupitia boti hizo wanashindwa kumudu gharama na kuweza kuwahudumia wananchi kama ilivyokusudiwa.

“tuengeomba kama kuna uwezekano Serikali ingeweza kutusaidia, kwa kutuingizia angalau Bajeti ya kuweza kufidia gharama hizo, pale zinapopungua kwa sasa inatuwiya vigumu kutokana na kuja nje ya bajeti zetu,“ alisema.

Akijibu masuala kutoka kwa kamati hiyo, juu ya nani mwenye dhamana wa kuzihudumia boti hizo, Afisa Mdhamini Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Pemba, Ibrahim Saleh Juma alisema jukumu kubwa la wizara yake katika hoti hizo, ilikuwa ni kazi ya ununuzi na baadae kukabidhiwa katika taasisi husika.

“Miundo na miongozo yote ya kuendeshwa kwa boti hizo, ziko chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za mitaa na Idara Maalumu za SMZ” alisema Mdhamini huyo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo Juma Ali Khatib, alisema kamati imeridhika na kikosi hicho katika kuzitunza boti hizo na kwamba, hatua za kuishauri Serikali juu ya namna ya uendeshaji zitachukuliwa.

Katika ziara hio kamati hiyo ilizitembelea boti za Makoongwe, Kisiwa panza, Fundo na Kojani ikiwa ni mfululuzi wa ziara yake ya kuitembelea miradi mbali mbali iliyogharamiwa na Serikali, ili kujua maendeleo yake pamoja na kuangalia namna ya fedha za Serikali zilivyotumika.