Monday, November 25

Waandishi ielimisheni jamii   juu ya kuzuia maambukizo ya VVU kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto-Mkurugenzi Mtendaji ZAC.

NA ABDI SULEIMAN.

 

AKINABABA wametakiwa kushiriki katika upimaji wa afya zao, wakati wenza wao wanapokuwa na ujauzito ili kumlinda mtoto na maambukizo ya virusi vya ukimwi, iwapo mmoja wao atagundulika kuwa na maradhi hayo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar Dk.Ahmed Mohamed Khatib, wakati akifungua mkutano wa waandishi wa habari juu ya kuzuia maambukizo ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto, uliondaliwa na shirika la Amref Health Africa Tanzania kupitia mradi wa afya kamilifu na kufanyika mjini Chake Chake.

Alisema kumekua na baadhi ya wamama hawapati mashirikiano na wenza wao, wakati anapokuwa wajanzito ikiwa ana VVU habaki kwenye huduma hali ambayo ni hatari kwa mtoto.

“Lengo la huduma hizi ni kuzuwia maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, ili mtoto atakaezaliwa awe salama na sio vyenginevyo,”alisema.

Aidha alisema mama ambaye huhuduria kiliniki na mwenza wake huwa anadumu vizuri katika huduma na mwenendo wake unaenda vizuri yeye na mtoto aliyemo Tumboni.

Hata hivyo alisema mpango mpango huo ulianza tokea 2005 huku vituo 177 Unguja na Pemba vipo vinavyotoa huduma hiyo, huku wanawake wote wanaohudhuria vituo vya afya kupima HIV.

Naye mratibu wa elimu ya mabadiliko ya tabia kutoka mradi wa afya kamilifu unaotekelezwa na Amref Health Tanzanzi, Sunday Beebwa alisema iwapo mama mjamzito anaeishi na virusi vya ukimwi atatumia dawa za ARV kikamilifu basi anaweza kuzaa mtoto ambae hana maambukizo.

Alisema iwapo mama atatutumia dawa vizuri kwa siku zote na kufuata maelekezo ya wataalamu na kuendelea kuhudhuria kliniki muda wote, hata wakati wa kujifungua ataendelea kupata ushauri wa wataalamu ataweza kumkinga mtoto asipate maamumbukizo na yeye mama ataweza kuimarisha kinga yake.

Hata hivyo aliwataka wananchi kuungana kwa pamoja katika kushajihisha akinamama wajawazito kwenda kliniki na wenza wao ili kuweza kumlinda mtoto na mama mjamzito kuepukana kupata maambukizo ya VVU.

Kwa upande wake Kaimu Mratibu wa Tume ya Ukimwi Pemba Ali Mbarouk Omar, aliwasisitiza waandishi hao kuendelea kuelimisha jamii juu ya kuzuia maambukizo ya vvu katika makundi mbali mbali.

Naye  Mratib wa Tume ya Ukimwi Zanzibar Sihaba Haji Saadat,  alisema jukumu la kuleta mabadiliko katika jamii ni la waandishi hivyo munapaswa kutumia vyema kalamu zenu katika kuelimisha jamii.