Saturday, March 15

“Wasaidieni wanawake wenzenu kuhakikisha wanasajili kisheria ardhi zao” Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya KUKHAWA

NA ABDI SULEIMAN.

IMEELEZWA kuwa kuanzishwa kwa kamati za ardhi katika shehia Kisiwani Pemba, zitaweza kusaidia kuondosha migogoro ya ardhi iliyokua ikitokea katika shehia.

Kuwepo kwa kamati hiyo migogoro ya ardhi itaweza kupungua na kitakacho tokea kitaweza kufuata sheria na taratibu katika utatuzi wake, ili kila mtu kupata haki yake kwa mujibu wa sheria za nchi.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya KUKHAWA Hafidh Abdi Saidi, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo kamati za ardhi za shehia juu ya umiliki wa ardhi kwa wanawake kisiwani Pemba.

Aidha alizitaja shehia zilizoshiriki katika warsha hiyo ni, Ole, Mfikiwa, Mvumoni, Gombani, Chonga, Mbuzini, Mgelema, Kilindi, Uwandani na Ngwambwa.

Alisema jambo la kusikitisha ni kuona wanawake ni asilimia 51% kwa mujibu wa sense ya 2012 lakini ni asilimia 31% wanaomiliki ardhi, hivyo wanapaswa kubadilika na kuendana na wakati kwani unapomiliki ardhi au shamba basi tayari umeshapiga hatua kubwa kimaendeleo.

“Changamoto nyingi zipo katika jamii juu ya masuala ya ardhi, nyinyi ndio wakuwasaidia wanawake wenzenu kuhakikisha wanasajili kisheria ardhi zao, kwani mafanikio yakipatikana yatakua mkombozi mkubwa kwao”,alisema.

Nao baadhi ya wanawake wameiyomba serikali, kuwaangalia wanawake wakati wa kugawa viwanja vyake kwa wale ambao wameomba, ili kuweza kuwainua kimaisha.

Bimkubwa Haji Hamadi mkaazi wa shehia ya Gombani, alisema wanawake wamehamasika sana kuomba viwanja katika maeneo ya serikali inapokata, lakini wanakuwa nyuma kupatiwa viwanja hivyo.

Sanoya Awadhi Mussa kutoka Uwandani alisema kikwao kikubwa kinachowapeleka kushidwa kusajili ardhi ni kutoana na gharama kubwa iliyopo kwa kamisheni ya ardhi Pemba.

“Wakati mwengine kiwanja kinafika laki saba hebu tizama mwanamke huyo pesa yote ataipata wapi, vizuri kupunguza bei ili na sisi tuweze kusajili”alisema.

Naye Anitha Kombo Ali kutoka mvumoni, alisema wakati umefika kwa taasisi za serikali na mashirika kupita vijijini kutoa elimu hiyo kwa jamii.

Mapema mkufunzi kutoka kamisheni ya Ardhi Pemba, ambaye ni mwanasheria wa Tasisi hiyo Asha Suleiman Sadi, alisema miongoni mwa mwambo yanayoepusha migogoro ya ardhi Zanzibar ni kuanzishwa kwa suala la autambuzi wa ardhi katika shehia.

Alisema suala la usajili wa ardhi bado imekua ni gharama kubwa kwa mwananchi, huku wananchi na viongozi wengi wamekosa uwelewa juu ya masuala ya ardhi.

Aliwataka wanawake kujitambua na kuamka kujuwa tahamani ya ardhi na mashamba yao, kwani vitu hivyo vinaweza kumuondosha na umasikini na kumsaidia hata kupata mikopo mikubwa.

Jumuiya ya KUKHAWA Pemba, imekua na kawaida ya kutoa elimu kwa wanawake makundi mbali mbali Kisiwani Pemba, juu ya kuhamasisha kusajili ardhi zao, ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa haki ya umiliki wa ardhi Pemba chini yaufadhili wa FCS na kufanyika mjini Chake Chake.