Monday, November 25

VYOMBO VYA HABARI VISAIDIE DUNIA KUPUNGUZA HOFU ZITOKANAZO NA HABARI POTOFU KWENYE MAPIGANO YA URUSI NA UKRAINE

Na Gaspary Charles.
Naiona hatari kubwa sana mbeleni ya athari za kisaikolojia ulimwenguni (world psychological effects by fake news) kutokana na kushamiri na kusambaa  kwa kasi sana taarifa potofu juu ya mapigano yanayoendelea kati ya Urusi na Ukraine.
Licha ya mzozo huu kufikia hatua mbaya sana, lakini ni wazi kwamba taarifa zisizo sahihi juu ya kinachoendekea Ukraine mpaka wakati huu ndizo zimechukua nafasi kubwa masikioni mwa watu hasa kupitia mitandao ya kijamii jambo linalozidisha  wasiwasi zaidi na taharuki kuwa kubwa zaidi duniani kuliko uhalisia wa jambo lenyewe lilivyo.
Kwa siku mbili mtawalia nimefuatilia kwa ukaribu vyanzo mbalimbali vya habari kutoka ‘viwanja vya mapigano’ na ni ukweli usiopingika kwamba hali kwasasa ni mbaya kwa maeneo hayo lakini zipo taarifa nyingi potofu na za uongo zinazoendelea kutengenezwa na kutumiwa kuuaminisha ulimwengu kuwa hicho ndicho kinachoendelea huko.
Na Bahati mbaya sana hata baadhi ya Vyombo vya Habari ambavyo ndio tegemeo la wananchi kupata taarifa sahihi juu ya kinachoendekea, vimekosa uhimilivu wa kuthibitisha taarifa zao kabla ya kuzirusha ( fact checking before airing/publishing) na badala yake vimejikuta vinaingia kwenye mtego mbaya sana wa kutoa taarifa zisizo sahihi na kuzidisha taharuki zaidi kwa walimwengu.
Ipo wazi kwamba nyakati kama hizi za taharuki ni kawaida na rahisi sana kutawala kwa ajenda ya habari feki, potofu na uongo (fake, misinformation and disinformation news) ambazo mara nyingi zote hutolewa kwa malengo mbalimbali mojawapo ikiwa ni kubadilisha ukweli na wakati mwingine ‘kuongeza chumvi’, rejea kipindi cha mripuko wa janga la Uviko 19.
Kipindi hiki ambacho nguvu ya mitandao ya kijamii imeshika kasi na kutawala sehemu kubwa ya maudhui ya kimatukio, ni muda mwafaka kwa vyombo vya habari kutilia mkazo suala la Uthibitishaji wa Taarifa zao ili kujinasua na mtego huu halamu.
Hii ni kutokana na kwamba Vyombo vya habari vinayo kazi kubwa sana kwasasa kutumia weledi wake kusaidia dunia kupunguza hofu na athari zote zitokanazo na taarifa za uongo/uzushi juu ya kinachoendelea huko.
Ni muhimu kutambua kwamba Uongo na uzushi hutengezwa na mtu au kikundi cha watu kwa lengo la kutimiza matakwa yao ya siri na kusambazwa na watu kwa kujua au kutokujua (mkumbo).
Wasalaaam.