NA SAID ABDARHAMAN.
MKUU wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar Zanzibar (JKU) Kanali Makame Abdalla Daima, amewataka maafisa wa Jeshi hilo Kisiwani Pemba kusimamia vyema miradi ya maendeleo, ili iweze kuleta ufanisi ndani ya Kikosi hicho.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imedhamiria kuwajengea wapiganaji wake makaazi yaliyo bora, pamoja na Kujenga Ofisi za kisasa katika makambi ya Vikosi vyake.
Daima aliyasema hayo huko Gombani Chake Chake Pemba, wakati alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake aliyoifanya Kisiwani huko hivi makaribuni.
Kanali Daima alisema kuwa ni vyema kwa maafisa hao, kushirikiana kwa pamoja katika kusimamia ujenzi wa Ofisi kuu iliyopo Chake Chake, ambayo inatarajiwa kujengwa ya kisasa pamoja na Ofisi na mahanga ya kulala Vijana huko katika Kambi ya Jku Chambani.
“Niwaombe muwe waaminifu katika miradi yetu hii, ili iweze kukamilika kwa wakati, unaotakiwa lakini iweze kuleta tija katika Kikosi chetu,”alieleza Kanali Daima.
Sambamba na hayo Kanali Daima, aliwasisitiza maafisa hao kuweka kumbukumbu za uhakika kwa kila ambacho kitaletwa kwa ajili ya majenzi hayo.
“Kubwa tuhakikishe kuwa tunaletewa vifaa kwa wakati na vile ambavyo tunavihitaji katika majenzi yetu,” alisema Kamanda Daima.
Kwa upande wa vituo vya wajasiriamali ambavyo wamekabidhiwa na Serikali, Kanali Daima alisema kuwa kazi imeshaanza kubwa ni kusimamia na kuhakikisha kazi hiyo, inafanyika kwa uharaka zaidi na iwe na ubora unaokubalika.
Mapema Mkuu wa Zoni Jku Pemba luteni Kanali Seif Omar Makwega alieleza kuwa kwa Sasa Zoni ya Pemba imeweza kutekeleza malengo ya Kilimo Cha mpunga katika Kambi ya Jku Msaani na kituo Cha Jku Kwapweza.
“Lakini pia tunaendelea na kilimo Cha mboga mboga kwenye makambi yote ya Pemba licha ya ukosefu wa maji kwa baadhi ya maeneo,”alisema Luteni Kanali Makwega.
Aidha Makwega alifahamisha kuwa kwa upande wa malezi ya vijana, wanaendelea kutoa mafunzo kwa vijana katika Kambi mbali mbali zilizomo ndani ya Zoni hiyo.
MWISHO