Friday, January 17

TAASISI YA NCA WANANCHI AMANI NDIO HADHINA PEKEE KATIKA DUNIA

AFISA Uchechemuzi na Mawasiliano kutoka taasisi ya Norwegian Church Aid Tanzania Nizar Seleman, akitoa taarifa fupi ya msafara wa vijana wa kuhamaisha amani na mtengamano wa jamii, kupitia mradi wa mtengamano wa jamii na amani Zanzibar, kwa wananchi wa Kisiwa cha Makoongwe Wilaya ya Mkoani, mradi huo ukiwa na kauli mbiu ‘’ Amani Yetu, Kesho Yangu’’

NA ABDI SULEIMAN.

TAASISI ya Norwegian church Aid Tanzania, imesema kuwa itaendelea kuhamasisha jamii katika suala zima la utunzaji wa amani, kwani ndio muhimili wa shughuli za kiuchumi kwa Taifa na jamii.

Hayo yalielezwa na Afisa Uchechemuzi na Mawasiliano Nizar Seleman Utanga, huko katika kisiwa cha Makoongwe Wilaya ya Mkoani Mkoa wa kusini Pemba, wakati wa mkutano wa msafara wa vijana wa kuhamaisha amani na mtengamano wa jamii kupitia mradi wa mtengamano wa jamii na amani Zanzibar unaotekelezwa na dini tafauti.

Alisema amani inapokosekana waathirika wakubwa ni wanawake na  Watoto, hivyo vijana, wazee wanapaswa kutambua kuwa ndio walinzi wakubwa wa amani hiyo iliyopo ambayo ndio tunu ya taifa.

Aidha alisema lengo la msafara huo ni kuhakikisha utunzaji wa amani na kutoa fursa kwa jamii, kuanzisha vikundi vya ushirika ambavyo vitatekeleza miradi ya uzalishaji ambayo itahimili mabadiliko ya tabianchi.

“Ushirikwaji huu ni kujenga amani na kuhamasisha wanawake na vijana kujiunga na kilimo kinachostahamili mabadiliko ya tabianchi ilikuweza kuondokana na hali ya umaskini”alisema.

Hata hivyo alisema msafara wa vijana kuhamasisha amani na utengamano wa jamii, unawaleta pamoja mabalozi wa amani vijana, vikundi vya taasisi ndogo za fedha za jamii, wanaume, wanawake, vijana, watendaji wa imani, viongozi wa dini, viongozi wa serikali, vyombo vya habari na taasisi ya fedha, asasi za kiraia.

Muakilishi kutoka taasisi za kidini zinazoshirikiana katika kutunza amani Zanzibar (ZANZIC) Profesa Issa Haji Zidi, amezitaka taasisi za kiraiya na serikali zimeshauriwa jenga amani wakati wa amani na sio kuisubiri wakati wa machafuko kwani lengo halitofikiwa katika jamii.

Alisema amani unagusa maisha ya kila mtu katika jamii, ikizingatiwa amani inahimiza maendeleo ya mtu mmoja mmoja nan chi kwa ujumla.

Kwa upande wake Afisa ushirika Wilaya ya Chake Chake Mwalimu Issa Ali, aliwataka wananchi wa Makoongwe kuanzishwa vikundi vya vikoba, kwani vinaleta tija kubwa katika kubadilisha maisha ya jamii katika shughuli za kiuchumi.

Alisema wakati umefika kwa vijana kujikusanya pamoja na kuunda vikundi vya ushirika, ili kuweza kuondokana na utegemezi sambamba na kuendelea suala zima la amani.

“Amani ndio kila kitu na ndio dira ya maendelea ya nchi, inapokosekana amani hakuna linaloweza kufanyika hata moja”alisema.

Akizungumza kwa niaba ya sheha wa shehia ya Makoongwe Khamis Saidi Massoud, aliwataka wananchi wa kisiwa hicho kuendeleza amani iliyopo nchini, sambamba na kupiga vita vitendo vya udhalilishaji.

MWISHO