Thursday, January 16

KUKHAWA YAWAFIKIWA WANAWAKE ZAIDI YA 5000 KATIKA MASUALA YA ARDHI PEMBA

NA ABDI SULEIMAN.

JUMUIYA ya Kupunguza Umaskini na hali za wananchi Kisiwani Pemba (KUKHAWA), imesema katika utekelezaji wa mradi wa Haki ya Umiliki wa Ardhi Pemba, imeweza kuwajengea uwelewa wanawake 5,800 huku wanawake 64 wameweza kupata ardhi kwa kipindi cha miaka mitatu 2019/2020 na 2021.

Akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya habari, katika ukumbi wa Jumuiya hiyo mjini Chake Chake, Mratib wa mradi huo kutoka KUKHAWA Zulekha Maulidi Kheir, alisema hayo ni mafanikio makubwa kufikiwa kwako.

Alisema wanawake hao waliweza kunufaika na sheria ya ardhi, njia za kumiliki ardhi, hatua na mambo ya kuzingatia katika kufungua kesi za madai ya ardhi na umuhimu wa kufanya mirathi mapema.

“Katika kuelekea siku ya wanawake maadhimisho ya wanawake duniani, KUKHAWA inaungana na wanawake wote duniani akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassana katika kuadhimisha siku hiyo”alisema.

Akizungumzia Changamoto Mratib huyo, alisema kasi ya wanawake kumiliki ardhi bado ni ndogo ukilinganisha na idadikubwa ya wanawake, pamoja na ugumu wa taratibu za usajili unaotokana na hatua nyingi na umbali wa ofisi ya kutoa huduma.

“Leo mtu wa Kisiwa Panza, Makoongwe, Micheweni wote hawa waje machomanne kusajili ardhi, ukizingatiwa mwanamke anamajukumu mengi ya kifamilia”alisema.

Aidha alisema gharama kubwa za usajili na hati za kuhodhi ni moja ya sababu inayopelekea wanawake, kuporwa ardhi zao kutokana na kutokua na ulinzi halali.

Aidha changamoto nyengine ni kuchelewa kwa hati baada taratibu kukamilika kutokana na idadi ndogo ya wateja katika kamisheni ya ardhi, hii inatokana na kuwepo kwa mtia saini mmoja wa hati kwa Zanzibar.

Akizungumzia dhamira ya KUKHAWA katika maendeleo ya wanawake, Zulekha alisema ni kuendelea kuwajengea uwelewa wanwake wote Pemba juu ya haki ya uliki wa ardhi na umuhimu wake katika maendeleo ya kiuchumi.

Alisema kutafuta fursa mbali mbali za kiuchumi kwa ajili ya wanawake, pamoja na kushirikiana na wadau wengine kuendelea kuhimiza utekelezaji wa haki za wanawake katika Nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Hata hivyo aliwataka wanawake wenzake kuwa mstari wa mbele kuhimiza haki zao, kushiriki kikamilifu shughuli za kimaendeleo ili kukwepa umaskini, kutunza utamaduni, mila na desturi za nchi.

Katika hatua nyengine alisema wakati umefika kwa serikali kutatua changamoto zinazokwamisha usajili na upatikanaji wa hati za ardhi, sambamba na wanaume kuacha mfumo dume unaolenga kumyima mwanamke haki ya kumiliki na haki za kujiendeleza kimeendeleo.

Nao waandishi wa habari waliweza kuipongeza KUKHAWA, kwa mikakati na juhudi zake za kuhakikisha inawakombo wanawake katika suala zima la upatikajani wa hati miliki za ardhi kisheria.

MWISHO