Monday, November 25

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Mhe Tony Blair Ikulu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Mhe.Tony Blair (kulia kwa Rais) akiwa na Ujumbe wake alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Mhe.Tony Blair, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na mgeni wake Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Mhe Tony Blair, wakizungumza na kuagana baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amempongeza Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Tony Blair kwa kutekekeleza kwa vitendo ahadi zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar hasa katika mipango na mikakati ya upangaji wa vipaumbele kwa watendaji wa Serikali.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Tony Blair Ikulu Zanzibar ambaye yupo Zanzibar kwa ziara maalum.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Waziri Mkuu Mstaafu Tony Blair kupitia taasisi yake ya (Tony Blair Institute for Global Change), imeweza kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kutoa mafunzo kwa watendaji wakuu juu ya upangaji wa vipaumbele hatua ambayo ina umuhumu mkubwa katika mipango ya Serikali.

Alisema kuwa mafunzo hayo ambayo Taasisi hiyo iliyatoa kwa watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yana mchango mkubwa  katika mipango ya Serikali na utekelezaji wake.

Aidha, Rais Dk, Mwinyi alimuhakikishia kiongozi huyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuthamini michango ya taasisi ya (Tony Blair Institute for Global Change), kwani imeonesha nia na dhamira kubwa ya kuiunga mkono Zanzibar ili mipango yake ya maendeleo iweze kufanikiwa ipasavyo.

Nae Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Tony Blair Ikulu Zanzibar alimueleza Rais Dk. Mwinyi hatua zinazoendelea kuchukuliwa na taasisi yake katika kuhakikisha malengo na mikakati ya kuiunga mkono Zanzibar yanatekelezeka na kuzaa matunda.

Tony Blair alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake anazozichukua katika kuhakikisha Zanzibar inapata maendeleo endelevu huku akimuahidi kuwa taasisi yake itaendelea kumuunga mkono.

Sambamba na hayo, Waziri Mkuu huyo mstaafu alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba tayari taasisi yake imeshaweka mipango kabambe katika kuhakikisha inatoa mchango mkubwa katika kuhakikisha mipango iliyopangwa na Serikali anayoiongoza Rais Dk. Mwinyi inatekelezeka.

Tayari taasisi ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Tony Blair (Tony Blair Institute for Global Change)  imeshatoa mafunzo ya Upangaji wa Viapaumbele kwa watendaji wakuu wa Serikali ya Mapiduzi ya Zanzibar wakiwemo Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Maafisa Wadhamini  pamoja na watendaji wengine, mafunzo yaliyofanyika mnamo mwezi wa Febuari mwaka huu huko katika ukumbi wa Chuo Cha Utalii Maruhubi, Zanzibar.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.