Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitamvumilia yoyote atakaejihusisha na matendo ya udhalilishaji kwa lengo la kumaliza kabisa tatizo hilo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt Hussein Ali Mwinyi ametoa kauli hiyo katika Hotuba iliyosomwa kwa Niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati akizindua Kongamano la Nane la kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
Amesema Serikali imejipanga na inaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wanaojihusisha na matendo hayo ambayo yanaiathiri jamii hasa kwa vizazi vijavyo.
Alhajj Dkt Mwinyi amesema imefika hatua kwa wananchi kuacha muhali na kutowaonea huruma wafanyaji wa vitendo hivyo ili kuisaidia Serikali katika kusimamia kesi za matukio hayo ya udhalilishaji.
Sambamba na hayo Rais Dkt Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwaasa waumini kujiandaa kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kuzidisha Ibada na kuacha yote yaliyokatazwa na Sheria yetu.
Kwa upande wake Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi amewataka waumini wa Dini ya Kiislamu kujikita katika Ibada kufikia Daraja la Uchamungu ambali ndio lengo la kuweko kwa funga ya Ramadhani.
Nae katibu Mkuu wa Taasisi ya Zanzibar Relief and Development Foundation (ZARDEFO) Ali Muhammad Haji ameeleza kuwa lengo la kuandaa Kongamano hilo ni kuwaweka tayari waumini kuweza kuukabili Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na kuwakumbusha waumini kuweza kujikita katika Ibada katika Mfungo mzima wa Mwezi wa Ramadhan.
Akiwasilisha Mada katika Kongamano hilo Alhabyb Muhammad Bin Hussein Alhabshy kutoka Seuni Hadhramut Nchini Yemen ameeleza kuwa ili kumaliza tatizo la Udhalilishaji ni vyema waislamu kurudi katika Sheria ya Allah Mtukufu.
Mada kuu katika kongamano hilo ni athari za udhalilishaji katika uislamu.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)