Friday, November 15

Mradi wa Wanawake na Uongozi Zanzibar wachukua sura mpya utatuzi vikwazo kwa wanawake

Mradi wa Wanawake na Uongozi Zanzibar wachukua sura mpya utatuzi vikwazo kwa wanawake
Washiriki wakiendelea na kazi za vikundi kuandaa mpango kazi.

 

(PICHA ZOTE NA TAMWA ZNZ)

 

WADAU wa haki za wanawake Pemba wamesema wapo tayari kushirikana na ofisi za serikali kujadili mbinu bora za utatuzi wa mapungufu na changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao na kupelekea kukwaza ufikiaji wa hazi za wanawake kushiriki kikamilifu katika masuala ya uongozi.

Wametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa kujadili mpango kazi wa namna ya kuzitaftia ufumbuzi changamoto zilizoibuliwa na wahamasishaji jamii kupitia mikutano iliyofanyika kwenye shehia  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ushiriki wa wanawake katia uongozi unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania, (TAMWA Zanzibar), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Pamoja na PEGAO kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Norway nchini.

Walisema baada ya kuzibaini changamoto hizo zilizopo katika jamii, watasaidia kuongeza nguvu kuzifikia taasisi zote zinazohusika na utatuaji wa kero hizo ili kushauriana njia bora za kutatua matatizo hayo.

Aidha walizitaka taasisi hizo ambazo zimeonekana kuwepo kwa changamoto katika utoaji wa haki kwa wananchi kuwa tayari kushirikiana na wadau hao ili kuzitaftia suluhu ya Pamoja changamoto hizo.

Safia Saleh Sultan, mhamasishaji jamii Wilaya ya Chake, alisema moja ya changamoto iliyoibuliwa ni uwepo wa sheria zinazokwaza ufikiaji wa usawa wa kijinsia kwa wanawake kushiriki katika ngazi za uongozi kutokana na sheria hizo kuweka masharti magumu kwa wanawake wanapohitaji kugombea.

Alitaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni; Sheria ya watumishi wa Umma No.3/2003, Sheria ya Mahakama ya Kadhi  No.7/2001, Sheria ya Vyama vya Siasa (1992) na Sheria ya Uchaguzi no 4/2018,  ambapo sheria hizo zimeweka masharti magumu kwa wanawake wanapohitaji kugomea nafasi za uongozi.

Alisema kutokana na masharti ya sheria hizo kuwa ngumu kwa wanawake watumishi wa umma inapelekea kukosekana kwa wanawake wenye uwezo mzuri wa kiutendaji katika ngazi za maamuzi.

Nae mhamasishaji jamii Wilaya ya Wete, Rukia Ibrahim, alisema kuwepo kwa wanawake wengi wasiojua kusoma na kuandika ni miongoni mwa changamoto pia zilizobaika kwenye shehia kuwakosesha wanawake kushiriki kikamilifu katika michakato ya kiuongozi.

Alieleza, “kutokujua kusoma na kuandika kwa baadhi ya wanawake wengi tulibaini ni changamoto inayokwaza wanawake wengi kukosa haki zao za kushiriki katika masuala ya demokrasia na uongozi.”

Mapema mkurugenzi wa jumuiya ya PEGAO, Hafidh Abdi, alisema mkutano huo ulilenga kuwaleta Pamoja wadau wa haki za wanawake kuzipitia changamoto zilizoibuliwa na wahamasishaji jamii kwenye shehia na kuandaa mpango kazi wa Pamoja kuhusu namna ya kutafta ufumbuzi wa changamoto hizo.

“Mkutano huu tumejikita kuzipitia changamoto zote zilizoibuliwa kwenye jamii  ambazo kwa namna moja au nyingine zinakwaza upatikanaji wa haki za wanawake na kuzijadili hapa kwa pamoja ili tuone ni njia gani bora tunaweza kuzitumia ili kusaidia changamoto hizo kutaftiwa ufumbuzi,” alisema Mkurugenzi huyo.

Changamoto nyingine ambazo ziliibuliwa na wahamasishaji jamii ni pamoja na, ukosefu wa vitambulisho vya mzanzibar na kuzaliwa kwa wanawake wengi, pamoja na huduma nyingine muhimu za kijamii ikiwemo maji safi na salama kwa baadhi ya shehia.

Mkutano huo uliwashirikisha wadau kutoka taasisi mbalimbali Pemba wakiwemo, viongozi wa vyama vya siasa, Dini, taasisi na idara za serikali, wasaidizi wa sheria, pamoja na asasi za kiraia zinazotetea haki za wanawake ambapo Pamoja na mambo mengine wliahidi kufanyia kazi changamoto zilizoelekezwa kwenye taasisi zao katika kipindi cha wiki mbili.