NA SAID ABRAHMAN.
WALIMU na Wanafunzi Kisiwani Pemba, wametakiwa kuvitumia vituo vya HUB ili waweze kujiendeleza kitaaluma.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Miradi kutoka taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Fatma Hamad, wakati akifungua mafunzo ya ELIMIKA yaliyoandaliwa na taasisi hiyo, kwa walimu wa Pemba huko katika kituo Cha HUB Kilichopo Skuli ya Sekondari Limbani Wete.
Alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha walimu kuweza kupata ujuzi wa kutumia mitandao, ili kuweza kuwafundisha wanafunzi kutumia njia ya mtandao katika masomo yao na kuwawezesha kufanya vizuri katika mitihani yao.
Aidha alifahamisha kuwa hivi Sasa mambo yamebadilika, hivyo aliwasisitiza walimu hao kuwashajihisha wanafunzi wao kutumia zaidi mitandao kwenye masomo yao.
“Walimu wangu kuvitumia hivi vituo vya HUB nyinyi na wanafunzi wetu, ili muweze kupata taaluma zaidi na kwa Sasa vituo vyetu vya Limbani, Pujini na Mtambile tayari “program” hii imeshaunganishwa, hivyo tembeleeni ili mujisomee,” alisisitiza Fatma.
Nae Mwalimu Shaame Faki Hamad kutoka Skuli ya Sekondari Fidel Castro, alisema kuwa katika mafunzo hayo wanatarajia kupata mambo matatu makubwa ikiwa ni pamoja na kupata fursa ya kutengeneza masuala kwa kutumia njia ya mtandaoni, kutengeneza kazi za madarasa yao pamoja na kupata taaluma ya ufundishaji wenye ubora zaidi.
“Kiukweli tutaweza kujifunza mambo mengi sana hapa, hivyo tutakapoondoka hapa tutakuwa wajumbe kwa wenzetu ambao hawakupata fursa hii,”alisema Shaame.
Nae Mwalimu Bahati Nassor Suleiman kutoka Skuli ya Sekondari Madungu alieleza kuwa matarajio yake katika mafunzo hayo ni kuweza kutumia mtandao.
“Naamini kutokana na malengo ya Milele Foundation ya kutaka kukuza elimu kwa wanafunzi wa Zanzibar, elimu hii nitaitumia ili kuhakikisha azma ya taasisi hiyo inafanikiwa kwa kiasi kikubwa,” alisema Bahati.
Hata hivyo Bahati aliwataka walimu wote ambao watapatiwa mafunzo hayo kushirikiana pamoja ili kutekeleza jambo hilo na kuitumia ipasavyo teknolojia kwa kumkuza mtoto wa kizanzibari kielimu.
Nae msimamizi mkuu wa kituo Cha HUB katika Skuli ya Sekondari Limbani Wete Abdalla Hamad Abdalla aliwataka walimu na wanafunzi wote kukitumia kituo hicho kwa ajili ya kupata taaluma mbali mbali za masomo yao.