NA SAID ABRAHMAN.
TAASISI ya Ifraj Zanzibar Foundation, kwa kushirikiana na Milele Zanzibar Foundation, imekabidhi msaada wa vyakula mbali mbali kwa ajili ya futari, kwa skuli sita Kisiwani Pemba za Sekondari Kisiwani Pemba.
Skuli zimepatiwa futari hiyo ni Skuli ya Sekondari Madungu, Fidel Castro, Pindua, Istiqama, Amini Islamic na Skuli ya Sekondari Dk.Salim Ahmed Salim.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi futari hiyo, kwa walimu wakuu wa skuli hizo, huko katika ofisi za Milele Zanzibar Foundation Mfikiwa Wilaya ya Chake Chake, Mkurugenzi wa taasisi Ifraji Zanzibar Foundation, Abdalla Said Abdalla alisema mwaka huu wamedhamiria kutoa futari kwa familia 4000 Kisiwani Pemba, ambazo zitaweza kuwasaidia katika mwezi wa Ramadhani.
Alisema taasisi ya Ifraji ifraji imekua ikisaidia kutoa msaada huo kwa familia mbali mbali, kila mwaka katika mwezi wa ramadhan ili kuwasaidia wale wasiojiweza.
Aidha alisema kutokana na Ugonjwa wa COVID 19 ulivyoweza kutikisa dunia kiuchumi, imepelekea hali kubadilika kidogo kulingana na miaka iliyopita wanavyotoa.
“Tumeweza kukabidhi mchele, unga wa ngano, unga wa sembe, sukari, maharage na mafuta ya kula, niwaombe tu wale ambao tulikuwa na mazoea ya kuja hapa Ofisini kutafuta chochote, kwa mwaka huu hapa itakuwa hakuna chochote mzigo wote utakaoletwa hapa tayari umeshafanyiwa hesabu yake,”Alisema.
Nae Ofisa Miradi Milele Zanzibar Foundation, Fatma Khamis aliziomba jumuia nyengine ambazo zina uwezo wa kusaidia jami, kwa kutoa misaada kwa wingi kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani.
Aidha Fatma aliwataka walimu na wanafunzi wa skuli hizo, kuhakikisha misaada hiyo wanaitumia kwa lengo lililokusudiwa na sio kuhifadhi pembeni na kupelekea familia zao.
Akitoa shukurani zake kwa taasisi hizo, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Istiqama Khamis Mohammed Saleh,alizishukuru taasisi hizo kwa msaada huo, huku wakiahidi kuutumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Aidha Mwalimu huyo alizitaka taasisi nyengine ambazo zina uwezo wa kusaidia kujitokeza na kuwasaidia, ili watoto wao waweze kupata futari katika kipindi hichi Cha ramadhan.
Nae Mwanafunzi Ali Hamad Juma kutoka Skuli ya Sekondari Dk.Salim Ahmed Salim, alisema msaada huo utaweza kuwasaidia kuondokana kuagizia chakula majumbani mwao.