Friday, November 15

Wanamtadao wa Kamati za kupinga udhalilishaji wanufaika na mradi wa DANIDA .

 

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WANAMTADAO wa Kamati za kupinga udhalilishaji Wilaya ya Wete na Mkoani wamesema, mafanikio mengi wameyapata katika mradi wa Jukwaa la Wanahabari la Kupinga Udhalilishaji, ikiwa ni pamoja na wananchi kupata mwamko wa kuripoti matukio hayo kwenye vyombo husika.

Wakizungumza wakati wa kufanya tathmini ya mradi huo unaofadhiliwa na DANIDA, wanamtandao hao walisema kuwa, kabla ya mradi wanajamii walikuwa wanaficha matukio hayo kutokana na kuona aibu.

Walisema kuwa, baada ya TAMWA kutoa elimu kwa jamii na kwenye kamati hizo, ilisaidia wanajamii kuripoti matukio ya udhalilishaji kwenye vyombo husika na kuyasimamia katika kuhakikisha kesi zao zinapata hatia.

“Watu wanasema matukio yamezidi, lakini hii ni kwa sababu wanajamii sasa wanaripoti, lakini zamani walipokuwa hawajapata hii elimu walikuwa wanayaficha kwa kuona aibu kuyaripoti”, walieleza wanamtandao hao.

Walifahamisha kuwa, wamekuwa wakitoa elimu kwa wanajamii na kuibua matendo ya udhalilishaji yaliowazi na yaliyojificha, kwa lengo la kupunguza ama kuondosha vitendo hivyo ambavyo vinawatesa wanawake na watoto.

Katibu wa mtandao Wilaya ya Mkoani Shaaban Juma Kassim alisema kuwa, mafanikio yameonekana sana kwani wamekubalika kwenye jamii na wameaminiwa, jambo ambalo limewasaidia sana kwani linapotokea tukio wanapewa taarifa na wanasaidia kufuatilia pamoja na wafamilia.

“Vita sio ndogo lakini tunahitaji, tunaomba mradi uendelee ili kupambana zaidi kwa sababu bado kuna changamoto ambazo zinahitaji zipatiwe ufumbuzi”, alieleza.

Nae Mwenyekiti wa mtandao huo Wilaya ya Wete Rashid Hassan Mshamata alisema kuwa, pamoja na mafanikio hayo kumekuwa na changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya wahanga kukataa kutoa ushahidi, jambo ambalo linasababisha kesi kufutwa.

“TAMWA kupitia mradi huu imekuwa ikiwaita wahanga na wazazi wao kuwapa mafunzo namna ya kwenda kutoa ushahidi mahakamani na nashkuru tumefanikiwa, lakini kuna wengi huko nje ambao hawajapata mafunzo, tunaomba na wao wapewe”, alisema.

Aidha alieleza kuwa, mitandao hiyo ya kupinga udhalilishaji imekuwa ikitoa elimu sehemu mbali mbali ingwa kwenye baadhi ya vijiji vya mbali na visiwani wanashindwa kufika kutokana na kukosa nyezo muhimu ikiwemo usafiri.

“Kwennye visiwa matukio ni mengi na tunapigiwa simu kuambiwa, lakini hatuna nyenzo za kutufikisha huko, tunawaomba wafadhili waendelee kuwasaidia TAMWA ili tuwezeshwe kufika huko kuwasaidia wanajamii wapate elimu ya udhalilishaji”, alisema.

Baadhi ya wazazi ambao walipata mafunzo namna ya kutoa ushahidi, walisema kuwa TAMWA imewasaidia sana kielimu kwani baadhi yao walikuwa wameshakata tamaa ya kuendelea na kesi zao, ingawa baada ya kupata mafunzo walihamasika na kuendelea kufuatilia.

“Kuna mwenzangu mmoja mtoto wake alibakwa lakini alipewa rushwa na kusema kuwa mtoto wake hajafanywa kitu chochote, lakini mimi nilisimamia mpaka mshitakiwa akafungwa”, alisema baba mmoja ambae mtoto wake wa darasa la nne alibakwa.

Aliwaomba wafadhili wa mradi huo ambao ni DANIDA waendelee kuwasaidia TAMWA, ili na wao wapate kuwazindua wanajamii ambao bado hawana mwamko wa kuripoti matukio hayo, ili elimu iwafikie wanavijiji wote.

Kwa upande wake mwanamtandao kutoka Wete Mwalimu Bakar alisema, vikao wanavyofanyiwa na TAMWA vinawapa ujasiri wa kufika sehemu mbali mbali ikiwepo Polisi, mahakamani na ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka kufuatilia kesi, jambo ambalo kabla ya mafunzo hawakupata uthubutu huo.

Nao waandishi wa habari walisema kuwa, wamepata mafanikio makubwa katika mradi huo kutokana na mafunzo waliyoyapata kwani yaliwawezesha kuibua matukio mbali mbali na kuyafuatilia na hatiame kupata hatia.

Nae Darius Cosmas kutoka Ubalozi wa Denmak kupitia mradi wa DANIDA aliwataka wanamtandao hao kuendelea kufanya kazi pasi na kuwezeshwa na TAMWA kwani wameshapata elimu, ni muhimu kuifanyia kazi kama walivyoelekezwa.

“Tutayafanyia kazi maombi yenu kuhakikisha tunaondosha vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa nguvu zote, lakini mjitahidi na nyinyi kufanya kazi ya kuelimisha jamii hata kama TAMWA haipo na nyinyi”, alisema Darius.

Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said aliwataka wanamtandao hao kushirikiana pamoja katika kuhakikisha wanaendelea kuibua matendo hayo na kuyafikisha kwenye vyombo vya sheria.