Friday, February 28

Mkurugenzi TAMWA-ZNZ ataka wanawake kujitokeza kugombea uongozi chaguzi za vyama zinazoendelea

Na Muhammed Khamis,TAMWA-ZNZ

Wakati baadhi ya vyama vya siasa Nchini Tanzania  vikiweka wazi tarehe za uchaguzi kupitia Jumuia zao Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ Dkt Mzuri Issa amewataka wanawake wa vyama hivyo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbali mbali za uongozi tangia ngazi za awali za uongozi.

Amesema  ni muhimu sana wanawake kushika nafasi za uongozi lakini wanapaswa kujipanga tangu mchakato wa nafasi za awali kuliko kusubiri kugombea nafasi za Ubunge na uakilishi huku wakijisahau kuwa walishindwa kujipanga awali na kutengeza mtaji wa kura za mwanzoni.

Kauli hiyo ya Mkurugenzi wa TAMWA imekuja siku chache baada ya Chama cha Mapinduzi CCM pamoja na ACT kutangaza uchaguzi za Chama ndani ya chama kupitia nafasi tofauti za Jumuia ndani ya Chama hicho huku wenzao ACT wakitangaza baadhi ya nafasi zilizowachwa wazi kutoka na sababu mbali mbali.

Alisema ili wanawake wengi waweze kushika nafasi za juu za uongozi hawana budi kujiimarisha mapema ikiwemo kugombe nafasi za matawi na majimbo kwa kuwa ndio kwenye mtaji mkubwa wa wapiga kura na kuacha kusubiri kugombea nafasi za juu huku wakiwa si watu wenye kujulikana na wanachama wenzao wala ngazi zengine za vyama wanavyogombea.

,, Ni lazima wanawake wafahamu kuwa uongozi hauji kama bahati ni nadra sana, lakini wanchopaswa kufanya ni kujipanga mapema ikiwemo kujitokeza kwa wingi hivi sasa kwenye chaguzi hizi za vyama vyao,,alisisitiza.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo alisema inawezekana baadhi ya watu kwa malengo yao wakajitokeza kukatisha tamaa wanawake watakao jitokeza kugombea nafasi hizo jambo ambalo alisema halipaswi kupewa nafasi na kuwataka viongozi wa vyama vya siasa kutoa fursa sawa kwa wananchama wao wote bila ya wanawake kubahuliwa au kuwekewa matabaka maalumu.

Akiendelea kufafanua zaidi alisema wanawake hawana sababu ya kuogopa ukizingatia walio wengi tayari wameshapewa elimu ya kutosha na kuhamasika na kufahamu mbinu mbali mbali ambazo zitawasadia kuwa viongozi na kukabiliana na changamoto watakazokutana nazo.

Aidha alisema wao kama Asasi za kiraia kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway Nchini Tanzania tayari wamefanya kazi kubwa ya uhamasishaji na kuwafikia wananchi wapatao 6917 ambao kati yao wanawake ni 4797  na wanaume 2120 katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba na kuna mafanikio makubwa ikiwemo uhamisikaji wa wanawake kugombe na wanaume kuwaunga mkono.

Akiendelea kufafanua zaidi alisema idadi hiyo ya watu iliofikiwa  ni mashirikiano ya wenzano wa PEGAO na ZAFELA  katika utekelezaji wa mradi ambao unalenga kuihamasisha jamii kumuunga mkono mwanamke kushika nafasi za uongozi ambao  mikutano hiyo ilifanyika ndani ya shehia 86 Unguja na Pemba  kwa Unguja mikutano ya kijamii ilifanyika katika shehia  zipatazo  45 na Pemba 41.

Wakati hayo yakijiri visiwani hapa baadhi ya wanachama wanawake wa chama cha Mapinduzi kutoka maeneo tofauti wamesema wamejipanga vyema na tayari wamechukua fomu za kugombea nafasi tofauti kupitia Jumuia zao.

Mmoja miongoni mwao Jine Kheri kutoka Kisiauni Wilaya ya Magharib B Unguja alisema amechukua fomu kushiriki katika uchaguzi wa nafasui ya Jumuia ya vijana akiamini kuwa kwa uwezo aliona atashidna nafasi hiyo.

Alisema kwa sasa hawezi kurudishwa nyuma ukizingatia amejengewa uelewa mpana zaidi na kufahamu kuwa haki ya kuwa kiongozi si wanaume tu bali hata wanawake wanapaswa kuwa viongozi.

Nae Hashim Abdalla wa Kiembe samaki mjini hapa alisema atahakikisha anawashawishi wajumbe wengine kuwaunga mkono wanawake watakaojitokeza kugombea nafasi zilizotangazwa na chama chao cha CCM akiamini kuwa wakati umebadilika na jamii haina budi kuwaunga mkono wanawake kushika nafasi za uongozi.

MWISHO